RC Mnyeti aagiza kukamatwa mwenyekiti wa CCM

Muktasari:

  • Mgogoro wa ardhi katika kitongoji cha Sukuro uliodumu kwa zaidi ya miaka kumi, umeelezwa kuchochewa na viongozi wa kisiasa hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi

Simanjiro. Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexanda Mnyeti amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula kuhakikisha Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Awadhi Omary anakamatwa na polisi na kulazwa mahabusu endapo ataendelea na mtindo wake wa kusababisha migogoro ya ardhi kwenye kitongoji cha Sukuro.

Mnyeti alitoa agizo hilo jana wakati akitatua mgogoro wa ardhi wa miaka 10 wa kugombea kitongoji cha Kitiangare kati ya kijiji cha Sukuro na Katikati wilayani Simanjiro.

Mkuu huyo wa mkoa, akizungumza mbele ya mkuu wa wilaya hiyo Chaula na Mwenyekiti wa CCM Omary, alimuonya kutokuwa kitovu cha kusababisha migogoro ya ardhi isiyo na tija.

“Mkuu wa wilaya hakikisha huyu Mwenyekiti wa CCM akiendeleza hii tabia ya kusababisha migogoro ya ardhi, agiza polisi wamuweke ndani kisha mnijulishe kuna sehemu ya kuwaweka watu kama hawa,” alisema Mnyeti.

Alisema awali, alipata taarifa Mwenyekiti huyo alifika siku moja kabla yake na kufanya kikao na wananchi kitongoji cha Kitiangare na kuwashawishi wakatae kwenda kijiji cha Sukuro wang’ang’anie Kijiji cha Katikati.

“Mwenyekiti nakuonya kwa mara ya mwisho ukirudia tena nitakuchukulia hatua kali.”

“Wewe unakuja kufanya mikutano huku kushawishi wananchi wakatae uamuzi wa serikali kule Mirerani nilikusamehe sasa hii mara ya pili rudia tena uone nitakukamata nikuweke ndani,” alisema Mnyeti.

Awali akizungumza  na wananchi wa kitongoji cha Katikati aliwashukuru kwa uvumilivu, busara  na hekima walizozitumia katika kupigania haki ya kitongoji chao.

“Ni zaidi ya miaka 10 sasa mgogoro huu wa ardhi umekuwa ni kero hii ni kutokana na siasa zisizoleta maendeleo hivyo kuwafanya wananchi kushindwa kuendelea kujikwamua kiuchumi  na haya ni majibu kutoka serikali kuu kitongoji cha Katikati kibaki katika kijiji cha Sukuro," alisema Mnyeti.

Hata hivyo, Omary alikanusha kusababisha mgogoro kwenye eneo hilo kwani yeye amekuwa msuluhishi na siyo mchonganishi.

“Mkuu wa mkoa amepewa taarifa potofu juu ya hilo kwani wilaya hii kuna baadhi ya viongozi siyo waaminifu na wametumia fursa hiyo kwa kutoa maelezo yasiyo ya kweli,” alisema Omary.

Mmoja kati ya wananchi wa eneo hilo, Abraham Koringo alipongeza uamuzi huo kwani baadhi ya viongozi walitumika kusababisha mgogoro huo uliodumu kwa muda wa miaka 10 pasipokuwa na sababu yoyote ile.

Mgogoro huo ulishawahi kusababisha ugomvi kati ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Christopher Ole Sendeka na aliyekuwa mkuu wa mkoa huo Henry Shekifu, ambao walirushiana maneno hadharani.