RC amsimamisha kazi mganga mfawidhi

Muktasari:

Baadhi ya tuhuma zinazoikabili Hospitali ya Kitete ni lugha chafu, rushwa na uzembe unaosababisha vifo


Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amemsimamisha kazi Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Kitete, Dk Nassoro Kaponta kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazoikabili hospitali hiyo  zilizotolewa na wananchi.

Uamuzi huo wa Mwanri ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa umetolewa leo Jumatatu Machi 19, 2018 baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati hiyo na wafanyakazi wa hospitali ya Kitete.

Mwanri amesema Dk Kaponta amesimamishwa sio kwa kuwa ametenda kosa, bali ni uwajibikaji wa kawaida kupisha kamati maalumu kufanya uchunguzi wa tuhuma  zilizotolewa na wananchi kuhusu mwenendo wa watumishi wa hospitali hiyo ambayo alikuwa akiisimamia.

Ametaja baadhi ya tuhuma hizo kuwa ni lugha chafu kutoka kwa baadhi ya wauguzi wanazotoa kwa wajawazito, wagonjwa kudaiwa rushwa na baadhi ya wafanyakazi na vifo wa akina mama vinavyotokana na uzembe.

Amebainisha kuwa licha ya kamati hiyo kuchunguza mambo ya kitaaluma, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Tabora imepewa jukumu la kuchunguza tuhuma zinazotolewa na wananchi kuhusu rushwa na lugha mbaya.

“Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu hospitali yetu ya mkoa…, tumeamua kumuweka pembeni mganga mfawidhi wa hospitali ili kupisha uchunguzi,” amesema Mwanri.

Amesema wakati uchunguzi ukiendelea Dk Kevin Nyakimori atakaimu nafasi ya kaimu mganga mfawidhi hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.

“Sitasita kuwachukulia hatua wauguzi na watumishi watakaowatoza fedha wajawazito, watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na wazee ambao inaagizwa wapate matibabu bure,” amesema.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Gunini Kamba amesema baadhi ya malalamiko ambayo yalifikishwa katika ofisi yake ni pamoja na kifo cha mfanyakazi wa Hazina Ndogo Tabora baada ya kufanyiwa upasuaji kutokana na utumbo kujikunja na mwanamke aliyekuwa na upungufu wa damu.