RC awageukia wafanyabiashara

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa

Muktasari:

Mlingwa alitoa onyo hilo  baada ya kufanya ziara ya kukagua hali ya chakula katika masoko manne mjini Musoma sanjari na kujua bei ya nafaka ambazo zinadaiwa kuwa adimu.

Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara wakubwa wanaodaiwa kuhodhi chakula ili wakiuze kwa bei ghali, baada ya kusambaza ajenda kuwa kimeadimika.
Mlingwa alitoa onyo hilo  baada ya kufanya ziara ya kukagua hali ya chakula katika masoko manne mjini Musoma sanjari na kujua bei ya nafaka ambazo zinadaiwa kuwa adimu.
Baada ya ziara hiyo,  mkuu huyo wa mkoa alitoa taarifa kwa waandishi wa habari bila kutaja mahitaji maalumu ya chakula kwa mkoa huo na kudai una ziada ya tani 461 ambazo zilivunwa msimu wa mwaka jana.
Mlingwa alisema katika msimu wa mavuno wa 2016 mkoa huo ulivuna zaidi ya tani 953,000 za chakula ambacho kitaendelea kutumika hadi Mei, mwaka huu na kwamba, licha ya ukame, lakini unatarajia kuvuna tani 193,000.