RC kuomba radhi kwa mwenyekiti CCM Taifa

Msimamizi wa uchaguzi wa jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), mkoa wa Mbeya ambaye pia ni mkuu wa mkoa huo, Amos Makalla akiandika dondoo zake kabla ya kuanza kwa uchaguzi wa jumuiya hiyo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Mbeya jana.

Muktasari:

Ni kwa kushindwa na Chadema katika uchaguzi mdogo Kata ya Ibighi

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amesema ataandika barua kwa mwenyekiti wa CCM Taifa na katibu mkuu wa chama hicho kuomba radhi kwa kushindwa kupata ushindi katika Kata ya Ibighi.

Kauli hiyo ya Makalla imekuja baada ya Chadema kupitia kwa mgombea wake, Lusubilo Simba kushinda kiti hicho kwa kupata kura 1,449 wakati Suma Fyandomo wa CCM alipata kura 1,205 kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika Jumapili.

“Nitaandika barua ya kukiomba radhi chama changu kwa katibu mkuu na mwenyekiti wake, lakini hapa ni lazima tujiulize ni kwa nini Mbeya,” alisema Makalla.

Makalla alisema hayo jana wakati akitoa salamu zake kwenye mkutano mkuu wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Mbeya ambao ulikuwa ni wa uchaguzi wa viongozi wa UWT ngazi ya mkoa akiwa kama msimamizi mkuu wa uchaguzi huo.

Makalla alisema kitendo cha CCM kushindwa katika uchaguzi kimeutia doa mkoa wa Mbeya na viongozi wa CCM mkoa huo wanapaswa kujitafakari upya kwa kilichotokea.

“Niseme tu hapa nimekuja tu kwenye mkutano huu kwa vile ni msimamizi mkuu wa uchaguzi huu, lakini ukweli hapa nilipo ninaumwa na jana (juzi) nilishindwa kufika kazini. Homa yenyewe inatokana na matokeo ya Kata ya Ibighi. Ni aibu kubwa kwa CCM mkoa wa Mbeya, tusidanganye hapa ni fedheha kata zote 43, halafu kata 42 zote zipo CCM na moja ndio imekwenda huko nayo ipo Mbeya,” alilalamika Makalla.

Kwa upande wake, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema hali ndani ya chama hicho mkoani hapa si nzuri kutokana na kitendo cha kushindwa kunyakua kata hiyo.

“Hali si nzuri kabisa wala tusifarijiane hapa, haiwezekani mkoa mzima una kata moja ya uchaguzi, halafu nayo tukapoteza. Ni bora hii kata moja ambayo CCM imepoteza ingekuwa kata nyingine lakini si Mbeya, hii inaonyesha kuna kazi ya kufanya,” alisema.

Dk Tulia alisema kupitia uchaguzi huo ni muda mwafaka wa kujitathmini na kuhakikisha wanarejesha imani kwa wananchi wa Mbeya na si vinginevyo, huku akibainisha kwamba si bure watu wakafanya uamuzi wa tofauti wakati wanatambua fika CCM ndio iliyoshika dola.

Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Mbeya, Mary Mwanjelwa alisema kwamba baada ya chaguzi zote ndani ya CCM kufanyika kimkoa ataanza kufanya kazi ya kuzunguka wilaya zote.