Raha na karaha za wafanyakazi kuhamia Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angellah Kairuki na Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Dk Laurean Ndumbaro wakiuaga msafara wa magari yaliyobeba vifaa vya ofisi vya kundi la kwanza la watumishi wa ofisi hiyo kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma, Januari 23, mwaka huu. Picha na Maktaba

Muktasari:

Kwa mujibu wa Majaliwa, ratiba ya Serikali kuhamia Dodom ilianza Septemba 2016 hadi 2020 wakati nchi itakapofanya uchaguzi mkuu.Awamu ya kwanza inayomhusisha yeye mwenyewe, mawaziri wote, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu wote na angalau idara moja ama mbili imeanza, Septemba hadi Februari 2017.

Wakati viongozi wanasema huduma za kijamii zimeboreka katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Serikali ihamie rasmi  mjini hapa, wakazi wanalia na hali mbaya ya biashara licha ya ongezeko la watu.

Rais John Magufuli alitangaza kuhamia mjini hapa katika Sikukuu za Mashujaa zilizofanyika kitaifa kwa mara ya kwanza mjini hapa tangu nchi ipate uhuru.

Uamuzi huo ulipokewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyetangaza ratiba ya zoezi la uhamiaji wa Serikali katika kipindi cha miaka mitano baada ya yeye mwenyewe kuhamia Septemba Mosi, 2016.

Kwa mujibu wa Majaliwa, ratiba ya Serikali kuhamia Dodom ilianza Septemba 2016 hadi 2020 wakati nchi itakapofanya uchaguzi mkuu.Awamu ya kwanza inayomhusisha yeye mwenyewe, mawaziri wote, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu wote na angalau idara moja ama mbili imeanza, Septemba hadi Februari 2017.

Awamu ya pili ni kati ya Machi 2017 hadi Agosti 2017 ambayo itawahusisha watendaji wa wizara mbalimbali.

Awamu ya tatu ni kuanzia Septemba 2017 hadi Februari 2018 na ya nne Machi 2018 na Agosti 2018.

Awamu ya tano ambayo ni Septemba 2018 hadi Februari 2020 itakuwa kuhamisha watumishi wa wizara waliobakia jijini Dar es Salam na ya sita ambayo itakuwa ya mwiso itakuwa ni kati ya Machi 2020 hadi Juni 2020 ambapo Ofisi ya Rais ikiongozwa na Rais, Makamu wa Rais watahamia mjini hapa.

Hata hivyo kutokana na baadhi ya ofisi kutokuwa na majengo yao, wizara sita zinalazimika kutumia majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom)  kwa muda wakati wakiendelea na utaratibu wa kujenga majengo yao.

Wizara hizo ni Katiba na Sheria, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Viwanda na Biashara, Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti madalali wa nyumba katika mji wa

Dodoma, walisema gharama za maisha zimeongezeka kwa kiasi kikubwa baada ya ujio wa Serikali mkoani Dodoma.

Mkazi wa Nkhungu, Salim Abdalah anasema kuwa gharama za maisha zimepanda katika maeneo mbalimbali ikiwemo vyakula katika migahawa.

“Mchemsho wa samaki ambao ulikuwa ukiuzwa Sh 4,000 sasa umepanda hadi kufikia Sh 6,000. Hali hii inafanya watu wa hali ya chini kushindwa kumudu gharama hizo,” anasema Abdalah.

Mkazi mwingine Easter Mwilima anasema kuwa kuku ambacho kilikuwa kitoweo kikubwa kwa watu wa Dodoma, sasa kinaanza kushindikana kununulika, bei imepanda.

“Kabla ya ujio wa Serikali kuku tulikuwa tukinunua kati ya Sh 8,000

hadi 10,000 lakini hivi sasa huwezi kupata kuku wa kienyeji kwa bei hiyo, ni mpaka uwe na Sh 12,000 hadi 15,000,” anasema.

Wafanyabiashara wanena

Mmoja wa madalali mashuhuri mjini hapa, Hechia Mangasta anasema nyumba katika maeneo mbalimbali ya mji ni kati ya Sh 400,000 hadi Sh 500,000 kutegemeana na uzuri na ukubwa wa nyumba.

“Lakini wageni wetu hawana uwezo wa kumudu bei hiyo, wanataka kwa Sh 200,000 lakini nyumba zipo nyingi hakuna shida hiyo,” anasema dalali huyo.

Dalali mwingine Hamis Alli anasema bei ya nyumba imeshuka kwa kiwango kikubwa kutokana na watu kutokuwa na fedha za kuweza kumudu mahitaji hayo.

“Nyumba ambayo ilikuwa ikipangishwa kwa Sh 300,000 sasa tunaipangisha kwa Sh 150,000 na kuna vijana walikuwa wakijenga nyumba unanua na kumalizia, walikuwa wakiziuza kwa Sh30 milioni sasa wanauza kwa Sh20 milioni,” anasema.

Anasema hata wateja wa kununua nyumba wamepungua na kwamba dalali ana nyumba 10 lakini akauza moja tu ndani ya mwezi mmoja tena kwa shida.

“Hata miezi ya kulipa pango (kodi) la nyumba imepungua, sasa wamiliki wa nyumba walikuwa hawataki kupokea kodi ya miezi sita lakini sasa wanapokea hata ya miezi mitatu, hali ni mbaya dada yangu tunapiga miayo tu hapa,” anasema.

Dereva wa teksi, Mathew James anasema wanaona watu wengi barabarani lakini hakuna ongezeko la wateja.

“Watu wanaona kuwa biashara imekuwa labda dereva bodaboda na bajaji, lakini kwa biashara ya teksi hali inazidi kuwa mbaya siku hadi siku,” anasema James.

Erick Fredrick ambaye ni dereva teksi, aliunga mkono kauli ya James kuhusu kupungua wateja.

Mmiliki wa Pub ya Cape Town inayojihusisha na utoaji wa huduma za chakula mjini hapa, Frank Ngonyani, anasema kumekuwa na ushindani tangu Serikali ihamie Dodoma.

“Nimejifunza kitu kimoja kuwa watu wanatakiwa kufanya kazi kwa juhudi kwa sababu zamani watu wamekuwa waki-relax (wakibweteka) sana lakini sasa ili upate mafanikio ni lazima ujitume sana,” anasema.

Naye Ofisa Mtendaji wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo Nchini (TCCIA) Dodoma, Fred Azaria anasema kumekuwa na uboreshaji wa miundombinu ya mji, hivyo kuongeza walaji katika biashara.

“Kumekuwa na ongezeko la viwanda vya kati tangu kutangazwa kwa Serikali kuhamia Dodoam, viwanda saba vya kati vinavyojishughulisha na usindikaji vimeanzishwa,” anasema.

Huduma za afya

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk James Kiologwe anasema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Serikali itamke kuhamia Dodoma kumekuwa na uboreshaji wa huduma za afya.

Anasema jengo la wanawake lililokuwa likihitaji kumaliziwa liweze kutumika, Serikali imeshatoa fedha zote zinazohitajika na litakamilika Septemba mwaka huu.

“Litabakia tu suala la furniture (samani) na vitu vingine ili liweze kuanza kutumika baada ya ujenzi kukamilika,” anasema.

Anasema katika Hospitali ya Kisasa ya Benjamin Mkapa ufungaji na upimaji wa vipimo vya MMRI na CT scan umeshaanza na hivyo kuondoa usumbufu wa wagonjwa wanaohitaji vipimo hivyo kwenda Dar es Salaam.

Huduma za umeme

Ofisa wa habari wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) mkoani hapa, Innocent Lupenza alisema katika mwaka wa fedha 2016/17, wamepeleka umeme katika maeneo maeneo mbalimbali ya mji na kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma hiyo.

Aliyataja maeneo hayo ni  Njadengwa, Ngongona, Ndachi, Stendi ya Mabasi ya Mkoa, Nzuguni, Chang’ombe , Mbwanga, Mcheula na Ilazo.

Alisema wateja wanaoelimishwa kulipia ni wale wanaohitaji nguzo mojahadi mbili ambao wamekuwa wakilipia na kuunganishwa huduma hiyo kwa gharama ya Sh 320,960.

“Maeneo yanayohitaji gharama kubwa kufikisha huduma tumeyaombea katika

miradio ya REA (Wakala wa Umeme Vijijini),”alisema Lupenza.

Alisema lengo waliloliwekea ni kuunganisha umeme kwa wateja wasiopungua 10,000 katika kila mwaka wa fedha, hatua ambayo wamefanikiwa kwa kuunganisha wateja zaidi ya lengo hilo kwa mwaka janawa fedha.

“Shirika limekuwa likitoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha kuwa tunatoa huduma nzuri kwa wakazi wote na wageni wanaohamia mjini hapa.

Tunapoomba vifaa vya kuwezesha kufikisha huduma tunavipata,” alisema.

Lupenza alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaopeleka maombi ya kuunganishiwa na wateja kutokana na kuongezeka kwa ujenzi wa nyumba katika maeneo mbalimbali.

“Hata katika viwanda tumepata maombi ya viwanda vitatu ambavyo vinataka kuunganishiwa huduma,” alisema Lupenza.

Hata hivyo, alisema pamoja na lengo kuwezesha wateja wanaomba umeme kupatiwa huduma hiyo, lakini baada ya ujio wa makao makuu walipeleka maombi ya fedha kwa ya uboreshaji wa huduma hiyo.

Alisema kwa upande wa umeme, wanao wa kutosha na mwingine unabaki licha ya mipango mbalimbali ya kuongeza uzalishaji.

“Sisi tuna Megawati 48 lakini matumizi kwa siku hapa kwetu(Dodoma) ni Megawati 28, tunabaki na Megawati 20 hivyo umeme wa kutosha upo hatuna shida,” alisema.

Huduma za maji

Meneja wa ufundi wa Duwasa wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa) Mhandisi Kashilimu Mayunga alisema Januari mwaka 2013 walianza utekelezaji wa mradi mkubwa wa uboreshaji wa huduma za maji.

Alisema mradi huo ulilenga katika uboreshaji wa chanzo cha maji cha Mzakwe, kuongeza uzalishaji wa maji, uwezo wa usafirishaji na uhifadhi.

Mayunga alisema mradi huo ulimalizika mwaka 2015 na ulifanyika kwa fedha Dola za Kimarekani 48.6 milioni na ulifanikiwa kuongeza lita za ujazo 30,000 kwa siku.

Alisema wanamatanki mawili ya kuhifadhia maji ambayo yapo Itega na Imagi na kwamba kukamilika kwa kumeongeza uwezo mkubwa wa utoaji wa huduma hiyo tangu mwaka 2016.

Mayunga alisema maji yaliyopo yanatosha kuhudumia watu watakaohamia kwa awamu ya tatu kwa sababu awali kabla uamuzi wa Serikali kuhamia mjini hapa mahitaji yalikuwa lita za ujazo 40 milioni kwa siku lakini hivi sasa ni 42 milioni.

Mayunga alisema katika bajeti yam waka 2016/17 waliongeza mtandao wa maji kwa kilomita 22  ili kuendana na mahitaji ya wakazi wa mjini hapa.

Aliyataja maeneo ambayo waliongeza mtandao wa maji kuwa ni Chidachi, Kinyambwa Extension, Miganga, Ndachi, Nkhungu, Mlimwa C, Nkalama, Mipango, Nzuguni.

Mayunga alisema katika mwaka huu wamepewa bajeti ya Sh1.04 bilioni kwa ajili ya kupanua mtandao wa maji katika maeneo ambayo bado hajafikiwa.

Hata hivyo, alisema ipo mipango ambayo imeanza kufanywa kwa ajili ya kuongezeka uzalishaji wa maji ambapo Serikali inajenga chanzo kipya katika bwawa la Farkwa.