Rahco yabisha hodi Kilimanjaro, kubomoa zaidi ya nyumba 100

Muktasari:

Nyumba hizo ambazo zimewekwa alama ya X na Rahco ikiwa ni operesheni ya nchi nzima kubomoa nyumba za waliovamia maeneo ya reli, zipo Mtaa wa Arabika, Kata ya Miembeni.

 Siku chache baada ya bomoabomoa inayoendeshwa na Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (Rahco) kutikisa mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma na Tanga, sasa ni zamu ya Kilimanjaro ambako zaidi ya nyumba 100 zimewekwa alama ya X ikiwa ni hatua ya awali ya kubomolewa.

Nyumba hizo ambazo zimewekwa alama ya X na Rahco ikiwa ni operesheni ya nchi nzima kubomoa nyumba za waliovamia maeneo ya reli, zipo Mtaa wa Arabika, Kata ya Miembeni.

Akizungumzia hatua hizo juzi, Ofisa Uhusiano wa Rahco, Catherine Moshi alisema watu wote waliovamia na kujenga maeneo ya reli lazima waondoke ili kupisha ujenzi wa reli.

Moshi alisema kampuni hiyo ilitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari Aprili 24 mwaka jana, kwamba watu waliovamia na kujenga maeneo hayo waondoke mara moja.

Alisema lazima wayachukue maeneo yao yaliyovamiwa na watu na kwamba, watahakikisha yamerudi mikononi mwa mamlaka husika kwa ajili ya kuendeleza reli.

“Watu walifikiri kwamba reli ilikufa ndiyo maana wakavamia na kujenga, lazima watupishe katika maeneo yetu ili tuyaendeleze na hii ni operesheni ya nchi nzima,” alisema Moshi.

Akizungumzia operesheni hiyo, Diwani wa Miembeni, Mbonea Mshana alikiri kuwapo nyumba zilizotangazwa na Rahco nchi nzima na kwamba, wote waliowekewa alama ya X wamepewa siku 30 kuondoka.

Hata hivyo, Mshana alisema amezungumza na ofisa mipango miji wa Manispaa ya Moshi kuona namna ya kushughulikia suala hilo.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi alisema hawajatoa hatimiliki na kuweka mawe ya mipaka maeneo hayo na kwamba, waathirika wameingizwa matatani na wahuni.

“Its very sad news (ni habari mbaya), reli hiyo ilikuwapo hata kabla ya uhuru. Watu hao waliingizwa mkenge (matatani) na wahuni, lazima atajulikana aliyefanya uhuni huo hata kama ilikuwa ni muda mrefu labda kama amekufa, lakini atajulikana tu,” alisema Mwandezi.

Machi 23, 2016 Rahco ilitoa notisi ya siku 30 kwa waliojenga kwenye maeneo ya reli kuondoka kupisha ujenzi wa reli ya Standard Gauge. Hata hivyo, Machi 11 ikiwa ni takriban mwaka mmoja kupita bila wahusika kubomoa kwa hiari, Rahco walianza kazi hiyo jijini Dar es Salaam na kuendelea mikoa ya Kigoma, Mwanza, Tabora na Tanga.