Raia wanne wa kigeni wachomwa kisu mgahawani Zanzibar

Muktasari:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Nassir Ali amewaambia waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumatatu kuwa tukio hilo lilitokea saa 1:20 usiku Jumapili.

Zanzibar. Watu sita wakiwemo raia wanne wa kigeni wamejeruhiwa vibaya kwa kuchomwa na  kisu usiku wa kuamkia leo katika mgahawa wa Lukman Mkunazi Mjini Zanzibar.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Nassir Ali amewaambia waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumatatu kuwa tukio hilo lilitokea saa 1:20 usiku Jumapili.

Kamanda huyo amesema kuwa mtuhumiwa aliyetenda tukio hilo  ambaye jina lake halijatambulika ila  kwa sura anafahamika, anakisiwa kuwa na umri wa miaka (25), lakini bado hajapatikana.

Amesema kuwa kwa mujibu wa uchunguzi wao wa awali wamebaini kuwa mtuhumiwa huyo alifika katika mgahawa huo na kuwachoma watu watatu ambao walikuwa  mgahawani hapo kwa ajili ya kujipatia chakula.

Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Mauget Gerarol (66) raia wa Ufaransa ambaye amejeruhiwa pembeni ya jicho la kulia, Jennifer Wolf (24) raia wa Ujerumani aliyejeruhiwa kichwani na Anna Catharina(20) raia wa Ujerumani aliyejeruhiwa kichwani pia.

Kamanda huyo alisema baada ya mtuhumiwa huyo kuwachoma visu watu hao alikimbia na akiwa njiani umbali wa mita 60 kutoka eneo la tukio la awali alikutana na vijana wengine waitwao Hassan  Abdallah mkazi wa Kiponda (24), Liying Liang ambaye ni raia wa Canada na kuwajeruhi kwa kuwachoma kisu mdomoni na shavuni.

Alisema alimchoma kisu pia Sajad Hussein  (55) na kwamba majeruhi hao wote walikimbizwa hospitali ya Tasakhtaa Global iliyopo Majestic kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Alisema kuwa  majeruhi hao wote walipatiwa matibabu na kuruhusiwa lakini Mauget Gerarol raia wa Ufaransa bado amelazwa hospitalini hapo na anaendelea kupatiwa matibabu.