Friday, November 10, 2017

Rais Botswana atangaza muda wa kung’atuka Ikulu

 

Gaborone, Botswana. Rais Ian Khama ametangaza kwamba atang’atuka Aprili 2018 muhula wake wa urais utakapoisha.

Khama alisema hayo alipolihutubia Taifa Jumatatu kwamba ataondoka na kuiacha nchi katika mikono ya Makamu wa Rais Mokgweetsi Masisi hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika 2019.

“Miezi mitano kuanzia sasa nitakuwa nakabidhi kijiti cha uongozi wa taifa hili mashuhuri kwenye mikono salama ya Makamu wa Rais Mokgweetsi Masisi. Wakati bila shaka yoyote tukiendelea kuzikabili changamoto muhimu, wakati tukitanguliza masilahi ya wananchi wa Botswana tutapata nguvu za kushinda vikwazo vyote,” alisema.

Khama alipanda kuwa rais mwaka 2008 akichukua nafasi iliyoachwa na Festus Mogae baada ya kuwa makamu wa rais tangu mwaka 1998. Alichaguliwa kuwa rais kwa muhula wa kwanza wa miaka mitano mwaka 2009 na akachaguliwa tena kwa muhula wa pili na wa mwisho mwaka 2014.

Nafasi nyingine ambayo kamanda huyo wa zamani wa jeshi ataachia pia ni ya kiongozi wa chama tawala cha Botswana Democratic Party (BDP) ambaye alichaguliwa Julai kuongoza chama hicho.

Kwa utaratibu huu Masisi ataongoza kama rais wa mpito hadi utakapofanyika uchaguzi mkuu mwaka 2019 ambapo atakabiliana na muungano wa vyama vinne vinavyolenga kuiondoa BDP iliyotawala Botswana tangu uhuru mwaka 1966.

-->