Rais Kenyatta:Sitamsaidia mgombea yeyote wa Jubilee

Muktasari:

Rais Kenyatta, alisema yeye kama kiongozi wa chama cha Jubilee, hatampendelea mgombea yeyote yule kila mmoja atajieleza mwenyewe akifuta kura kwa wananchi.

Kiambu. Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amewataka wagombea wa ubunge na nafasi mbalimbali wajitokeze wenyewe kujitetea mbele ya wananchi kuelekeza walichowafanyia wakati wa utawala wao.

Rais Kenyatta, alisema yeye kama kiongozi wa chama cha Jubilee, hatampendelea mgombea yeyote yule kila mmoja atajieleza mwenyewe akifuta kura kwa wananchi.

‘’Mimi hakuna mgombea yeyote nitakayempendelea hivyo yule atakayechaguliwa kwa haki katika uteuzi wa chama ndiye nitamuunga mkono,” alisema Kenyatta, na kuongeza kwamba hataki kiongozi yeyote atumie jina lake ili kujitafutia kura.

Alisema hayo katika jimbo la Kiambu alipoenda kuwahimiza wananchi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura.

Kenyatta alitembelea maeneo ya Thika, Gatundu na Githurai huku akisimama kwenye vituo hivyo akizungumza na wananchi waliofika kwa wingi kumshangilia.

Wakati wa ziara hiyo hakuna kiongozi yeyote aliyepata nafasi ya kusalimia wananchi kwani rais alijua hiyo ingeleta uhasama kati ya viongozi tofauti waliojumuika katika msafara huo.

Mahasimu wawili wa kisiasa William Kabogo na Ferdinand Waititu wote walikuwa katika msafara huo lakini hakuna yeyote aliyepata nafasi ya kujitambulisha kwa wananchi.

Viongozi wengine ni Mbunge wa Thika Alice Ng’ang’a, Patrick Wainaina, na Morris Mburu wote wanapigania kiti cha ubunge cha Thika.

“Mimi sina kiongozi yeyote ninayempendelea kwa hivyo yule ambaye wananchi wataniletea ndiye tutafanya naye kazi,” alisema Kenyatta.

Wiki mbili zilizopita Rais Kenyatta alitembelea eneo la Mlima Kenya kwa lengo la kulinda kura za eneo hilo na pia kuwahimiza kujiandikisha kwa wingi Baadhi ya maeneo aliyotembelea ni Murang’a, Nyeri, Laikipia, Meru, Embu, Thika, na Gatundu Kusini.

Washika dau wote, viongozi wa tabaka mbalimbali na machifu tayari wamepewa kibarua kikali cha kutafuta kila mmoja ambaye hajajiandikisha kuwa mpiga kura kufanya hivyo.