Rais Magufuli atangaza uamuzi mgumu Mererani

Muktasari:

  • Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa barabara mpya ya lami kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) hadi Mererani, yenye urefu wa kilomita 26, iliyogharimu Sh32.5 bilioni, Rais Magufuli alisema lengo la mpango huo ni kudhibiti wizi na utoroshwaji wa madini ya Tanzanite.

Mererani. Rais John Magufuli ameliagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujenga uzio kuzunguka machimbo ya Tanzanite Mererani, hatua ambayo imepokewa kwa hisia tofauti na wananchi wa eneo hilo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa barabara mpya ya lami kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) hadi Mererani, yenye urefu wa kilomita 26, iliyogharimu Sh32.5 bilioni, Rais Magufuli alisema lengo la mpango huo ni kudhibiti wizi na utoroshwaji wa madini ya Tanzanite.

Rais Magufuli aliagiza kuanza haraka kwa ujenzi huo kuzunguka eneo lote la migodi kuanzia Kitalu A hadi D lenye ukubwa wa kilomita za mraba kati ya 13 hadi 14 kwa kuwa ndilo lenye uzalishaji mkubwa wa Tanzanite.

“Lile eneo la Kitalu A hadi D ambalo ndilo lina mali nyingi ya Tanzanite naagiza Jeshi la Wananchi kupitia Suma JKT na wengine, najua wamekwishamaliza utafiti, waanze kujenga ukuta wataweka kamera na patakuwa na mlango mmoja, vifaa maalumu vya ukaguzi, wewe ukiweka Tanzanite tumboni tutakubaini ukiweka kwenye kiatu utaonekana pia,” alisema.

Alisema madini ya Tanzanite yamekuwa yakiibwa na kuonekana migodi hiyo ni shamba la bibi kutokana na watu wachache kuchukua madini hayo na kuondoka huku wakiwaacha wakazi wa Mererani na Watanzania wakiendelea kuwa maskini kwa kuambulia asilimia tano tu.

Rais Magufuli alisema ujenzi wa ukuta huo utawezesha Tanzanite yote inayochimbwa kujulikana hivyo, Serikali kupata malipo stahiki na pia mchimbaji atapata haki yake.

Alisema Serikali inataka kuhakikisha soko la madini ya Tanzanite badala ya kufanyika Arusha, linakuwa Mererani kwani kuna barabara ya lami na ni jirani na Kia.

“Wananchi wa Mererani pia watafanya biashara, wenye nyumba za kulala wageni watapata wageni, wauza nyama Wamasai watauza na hivyo maisha ya wananchi yatakuwa bora zaidi,” alisema.

Alisema katika eneo hilo la uzio, pia kutakuwa na maeneo ya kununua madini na kuitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuanza mkakati wa kununua madini hayo Mererani.

Mkataba wa Tanzanite One kutazamwa upya

Pia, Rais Magufuli aliiagiza kamati inayoongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kupitia upya mkataba wa Tanzanite One.

“Wakae watengeneze mkataba wenye faida, hatuwezi kuwa na mkataba wa kinyonyaji,” alisema.

Hadi jana, vyombo vya usalama vilikuwa vinawahoji maofisa wanne wa kampuni ya Tanzanite One, wakiwamo wakurugenzi wawili, Faisal Shabhai na Hussein Gonga.

Maoni ya wananchi

Hatua hiyo ya Serikali imepokewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wakazi wa Mererani.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Wamiliki wa Viwanda na Kilimo (TCCIA) Wilaya ya Simanjiro, Simba Willy alisema anaunga mkono uamuzi huo kwani ndicho walichokuwa wamependekeza katika Tume ya (Jaji Mark) Bomani.

“Sisi tunaunga mkono kuwekwa uzio Mererani kwani itadhibiti kutoroshwa madini na itarahisisha ulipwaji wa kodi za Serikali,” alisema.

Pia, mkazi wa Mererani, Baraka Kanunga alimpongeza Rais kwa mikakati yake ya kusaidia madini ya Tanzanite kuwanufaisha Watanzania wote, wakiwamo wachimbaji wadogo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara, Sadiki Mnenei alisema ujenzi wa uzio utatumia gharama kubwa na inawezekana usiwe na faida kubwa.

“Rais ana nia nzuri lakini ukuta ulishawahi kujengwa na haukusaidia kitu, mimi nadhani wachimbaji wakisimamiwa kufuata sheria, wakipata madini wanapaswa kumwita ofisa madini kukagua mgodini na baadaye kulipa kodi. Hii itazuia sana utoroshwaji wa madini,” alisema.

Kauli yake iliungwa mkono na mchimbaji maarufu kama mwanaApollo, Julias Laizer aliyesema uzio huo utawapa shida wanaochekecha mchanga uliotumika.

“Hii ya ukuta kaka ni ngumu sana, sisi huwa tunachekecha michanga tu na kupata kati ya Sh50,000 hadi Sh300,000 sasa tukidhibitiwa ina maana tutashindwa kuchekecha na wengine migodi yetu haijatoa madini muda mrefu hii itakuwa shida,” alisema.

Mbunge wa Simanjiro (Chadema), James Ole Millya aliunga mkono hatua ya Rais kuhakikisha biashara ya Tanzanite inawanufaisha Watanzania wote hasa wakazi wa Mererani ambao ni masikini, “Ni aibu madini ya Tanzanite kutoka hapa Mererani lakini bado wananchi ni maskini, wanaishi maisha duni, hakuna maji, wala huduma bora za afya.”

Katika hilo, Millya alimchongea kwa Rais, kiongozi mmoja wa CCM akisema amepora ardhi ya wananchi na akamuomba amchukulie hatua.

Bila kumtaja jina, Ole Millya alisema, “Mheshimiwa Rais tunashukuru sana kwa kuja hapa na wewe umesema maendeleo hayana chama. Naomba ushughulikie tatizo hili la wananchi kupokwa ardhi. Kuna mwenyekiti wa CCM amechukua ardhi ya wananchi na kujimilikisha sasa tunaomba uweke mkono wako ili tabia hii ikome.”

Mbunge wa Ngorongoro, William ole Nasha ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, alisema maisha ya wakazi wa Mererani hayaakisi utajiri wa madini ya Tanzanite ambayo yanapatikana Mererani pekee duniani.