Rais Shein aelezea mafanikio ya utalii Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein akizungumza wakati wa ufunguzi wa tamasha la utalii linaloendelea kwa siku nne Visiwani humo.

Muktasari:

  • Tamasha la utalii linaendelea visiwani Zanzibar kuanzia leo Oktoba 17 hadi 20, 2018 likikutanisha watalii 3,000 kutoka nje ya nchi na waonyeshaji zaidi ya 150.
  • Tamasha hilo litatoa fursa ya kuutangaza zaidi utalii ambao ndiyo nyenzo kuu ya uchumi visiwani Zanzibar ukichangia asilimia 27 ya pato la taifa la Zanzibar na asilimia 80 ya fedha za kigeni zinazokusanywa.

Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema siku za kukaa watalii visiwani humo zimeongezeka kutoka siku sita na kufikia nane.

Pia, imesema kuongezeka kwa takwimu hizo kunatokana na sekta ya utalii kukua kwa kasi na watalii kupenda kubakia nchini wakitumia fedha walizokuja nazo ambazo huchangia asilimia 80 ya fedha za kigeni zinazokusanywa.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Oktoba 17, 2018 na Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein alipokuwa akizindua tamasha la kwanza la utalii.

Amesema takwimu hizo ni njema kwa Serikali, wananchi, wawekezaji na wadau wote kwa kuwa zinabainisha sekta hiyo imekuwa.

Amesema juhudi mbalimbali za kuimarisha utalii zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ikiwamo kuanzisha mpango wa "utalii kwa wote".

Rais Shein amesema lengo la mpango huo ni kuhakikisha sekta hiyo inawanufaisha wananchi wote wa Zanzibar na kuimarisha ustawi wao kiuchumi.

"Maonyesho haya ni njia bora na madhubuti ya kutangaza Zanzibar na fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wawekezaji," amesema.

"Yatatoa fursa adhimu kwa washiriki kufahamu fursa zilizopo nchini hivyo washiriki changamkieni fursa hizo," amesema Dk Shein.

Amesema Serikali inaendelea kufanya juhudi ya kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kuzijenga upya na kuzifikisha katika maeneo muhimu ya utalii kwa lengo la kuimarisha sekta hiyo sambamba na shughuli za uwekezaji na utoaji huduma kwa wananchi.