Rais wa Liberia aacha ujumbe wa amani

Muktasari:

Amesisitza kwamba nchi hiyo ya Afrika Magharibi haipaswi kurudi zama za migogoro.

Rais anayemaliza muda wake Ellen Johnson Sirleaf amesema Waliberia wana wajibu wa kuhakikisha wanadumisha amani iliyopo waliyoifaidi kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita.

Akizungumza katika mahojiano na shirika la BBC, rais huyo mwenye umri wa miaka 78 na ambaye ni mwanamama wa kwanza kushika wadhifa huo barani Afrika, amesisitiza kwamba nchi hiyo ya Afrika Magharibi haipaswi kurudi zama za migogoro.

Alisema mgogoro uliwarudisha nyuma miongo kadhaa na ni Waliberia walioamua kukaa kwa amani.

Alipoulizwa ni ujumbe gani anaowapatia wananchi wake, alijibu: “Dumisheni amani, tusirudi nyuma kule kwenye migogoro. Nchi yetu ilirudishwa nyuma kwa zaidi ya miaka 30 kwa sababu ya migogoro. Jambo kubwa la kujivunia tulilofanya ni kudumisha amani na wala haikuwa rahisi.

 “Nilichukua juhudi kubwa kusimamia, kuvumilia, maridhiano na kila kitu kilichotuhakikishia amani kwa sababu bila amani tusingefanya haya tauliyonayo. Lakini leo nimefurahishwa mno, kizazi cha watoto wetu kinaweza kusema hakijui chochote kuhusu bunduki, hawana haja ya kukimbia.

“Na nafikiri watu wa Liberia wanashukuru leo (kwamba) wana uhuru wa kuzungumza, wanaweza kusimamia ndoto zao, hawana wasiwasi na kuna matumaini makubwa siku zijazo.”

Mwanamama huyo alisema anafurahi kwamba amezingatia sana katiba na atang’atuka mwezi ujao wakati Waliberia watakapomchagua mrithi wake. Alifurahi kutimiza wajibu mkubwa wa kuirejesha nchi katika mkondo wa demokrasia na maendeleo.