Ripoti ya makinikia yajadiliwa wiki nzima

Muktasari:

Ushauri wa jinsi ya kushughulikia suala hilo, pongezi, tamko la kutaka viongozi wa Serikali zilizopita wasihusishwe na sakata hilo, kufungia gazeti kwa kukiuka tamko hilo, uamuzi wa kuanzisha mazungumzo ya kutafuta suluhu, vijembe na maazimio ya Bunge kupongeza vita dhidi ya wezi wa rasilimali za nchi, vilitawala mijadala ya kuanzia Jumatatu hadi jana.

Unaweza kusema Juni 12 hadi Juni 17 ilikuwa ni wiki ya sakata la mchanga wa madini, ndani na nje ya Bunge.

Ushauri wa jinsi ya kushughulikia suala hilo, pongezi, tamko la kutaka viongozi wa Serikali zilizopita wasihusishwe na sakata hilo, kufungia gazeti kwa kukiuka tamko hilo, uamuzi wa kuanzisha mazungumzo ya kutafuta suluhu, vijembe na maazimio ya Bunge kupongeza vita dhidi ya wezi wa rasilimali za nchi, vilitawala mijadala ya kuanzia Jumatatu hadi jana.

makinikia bungeni. Pongezi, ushauri na mapendekezo yametolewa ili kuongeza tija ya sekta ya madini nchini baada ya Rais John Magufuli kupokea ripoti ya kamati ya pili kuhusu sekta hiyo.

Ilikuwa ni baada ya Rais John Magufuli kupokea ripoti ya kamati ya pili iliyoundwa kuchungua athari za kisheria na kiuchumi kuhusu usafirishwaji wa mchanga wa madini kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuyeyuishwa ili kupata mabaki ya dhahabu na madini mengine.

Ripoti hiyo ilipokelewa Jumatatu katika hafla iliyofanyika Ikulu na kurushwa moja kwa moja na vituo vya redio, televisheni na mitandao ya kijamii, huku viongozi wa dini wakifanya sala na wasanii wakitumbuiza wimbo wa uzalendo.

Licha ya kutofautiana kulikojitokeza wakati wa kuchangia azimio hilo, mwisho wa siku Bunge liliunga mkono hatua zilizochukuliwa na Rais Magufuli kukabiliana na udanganyifu unaofanywa kwenye sekta ya madini na kumhakikishia ushirikiano wakati wowote atakapohitaji.

Vilevile, liliishauri Serikali kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kushiriki kulitia Taifa hasara kutokana na kuidhinisha mikataba mibovu na kufanikisha wizi uliofanywa kwa takriban miongo miwili.

Ilitokana na pendekezo la mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga kulitaka Bunge kuunga mkono juhudi za Rais na kufanikisha kuipitisha hoja hiyo iliyoundiwa kamati na Spika Job Ndugai.

Baada ya Bunge kuridhia, mbunge wa Newala Mjini (CCM), George Mkuchika alipewa jukumu la kuongoza taratibu za kukamilisha suala hilo kabla hajawasilisha azimio lililopitishwa muda mfupi, kabla wabunge hao hawajaviacha viti vyao na kwenda kufuatilia ripoti ya pili kwenye televisheni.

Akihitimisha hoja yake, Mkuchika alisema: “Bunge linamuunga mkono Rais Magufuli na lipo tayari kutoa ushirikiano wa dhati kadri itakavyohitajika kuhakikisha juhudi hizi hazipotei bure na sekta ya madini inachangia maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.”

Ni wiki ambayo wabunge wanaotoka maeneo yenye migodi walionyesha kuguswa na wizi pamoja na udanganyifu unaofanywa na wawekezaji. Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche aliitaka Serikali iruhusu wananchi kuyalinda maeneo hayo.

Alikiri kwamba wananchi waliokuwa wanaiba mchanga huo kwenye mifuko ya kilo 50 kutoka katika malori, walikuwa wanapata mpaka Sh47 milioni baada ya kuuchenjua kwa njia za kienyeji.

“Watu wa Tarime wameumizwa, wamelizwa hata kuzika ndugu zao kutokana na suala la madini. Sasa imedhihirika kwamba Acacia imekuwa ikiwaibia Watanzania. Hakuna mfumo wa kukamata mwizi. Tunawadai fidia nyingi, tulitarajia Rais atazuia hata usafirishaji wa madini nje ya nchi,” alisema Heche.

Naye mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige alisema ipo haja ya kuweka misingi imara itakayowashirikisha wananchi kuimarisha mapato yatokanayo na madini.

Wakati taarifa za awali zikisema Acacia wamekubali kujenga mtambo wa kuyeyusha mchanga huo nchini pamoja na kulipa gharama nyingine zitakazokubaliwa kwenye mazungumzo yatakayofanyika, alipendekeza ujengwe maeneo yenye migodi.

“Tunaomba (mtambo wa kuchenjua madini) smelter ijengwe maeneo ambako Bulyanhulu ilipo. Tuambieni ardhi kiasi gani inahitajika ili tuanze kufanya maandalizi. Sitarajii smelter itajengwa sehemu nyingine zaidi ya Kahama,” alisema Maige.

Wakati ripoti hiyo ikisema Tanzania imepoteza Sh108 trilioni katika miongo takriban miwili ya usafirishaji mchanga nje na kwamba Acacia wamekubali kulipa, Maige alishauri halmashauri za Kahama na Msalala zilipwe fedha mrabaha mlabaha zinazodai ambazo ni kati ya Sh795 bilioni na Sh2.283 trilioni kwa uzalishaji wa migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi kati ya mwaka 1998 hadi 2017.

“Fedha hizi ziwemo kwenye majadiliano na tuzipate,” alisisitiza akijenga hoja kuwa halmashauri hizo pia zimepoteza haki hiyo katika wizi huo.

“Halmashauri zinadai Sh1.320 trilioni ya Corporate Social Responsibilities (huduma kwa jamii). Hili nalo lizingatiwe na halmashauri zipate haki yake.”

Naye mbunge wa Geita, Joseph Musukuma alijikita kwa wabunge na watendaji wengine wa Serikali waliotajwa kwenye ripoti hiyo, akitaka wafikishwe mahakamani haraka.

“CCM si kichaka cha kuficha wezi. Magereza hayajawekwa kwa ajili ya akina Babu Seya pekee. Ifike mahali tuambizane ukweli na tuache mzaha. Kuna watu wameumia sana kwenye suala hili. Waliotajwa wakamatwe,” alisema Musukuma.

Alisisitiza kwamba watu wanaotajwa kwenye kila tuhuma wanastahili kuchukuliwa hatua kwa kuwa hawana kinga yoyote.

Licha ya Musukuma kutaka kufikishwa mahakamani kwa waliotajwa, wapo ambao hawajashtushwa na hilo. Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye pia ni mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja alishindwa kujizuia.

“Kutuhumiwa si kukutwa na kosa. Maisha lazima yaendelee,” alisema baada ya mchango wake kukatizwa na mbunge aliyetoa mwongozo akieleza kutajwa kwake katika ripoti hiyo.

Ngeleja hayupo peke yake. Tayari Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amewazuia waliotajwa katika ripoti hiyo kusafiri nje ya nchi kusubiri kuhojiwa.

Masharti ya kufanikisha mazungumzo hayo kati ya kampuni ya Acacia na Serikali yalitolewa pia na mbunge wa Kiteto, Emmanuel Papian. Hii ni baada ya Rais Magufuli kufanya hivyo alipokuwa anapokea ripoti ya pili.

Wakati Rais alisema kampuni hiyo inapaswa kukiri kwa ilichofanya ili mazungumzo yafanyike, mbunge huyo ametaka kwanza Acacia itoe fedha za kishika uchumba.

“Kabla mazungumzo hayajaanza, Acacia walipe kwanza walau Sh35 trilioni za commitment fee. Hii itaongeza heshima kwa nchi yetu,” alisema Papian.

Hakuna mbunge anayepinga vita hivyo, lakini wapo wanaotahadharisha na kuhitaji ushirikishaji wa Watanzania wote bila kujali tofauti ya itikadi.

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alisema mchango wa Watanzania wenye taaluma tofauti unahitajika ili kuongeza tija na kufanikisha kuongeza mapato ya Serikali na kuinua uchumi wa Taifa na wananchi kwa ujumla.

“Vita vya kiuchumi ni vibaya sana. Hakuna mpinzani anayeshabikia wizi wa rasilimali zetu na ieleweke, vita hivi havihitaji ushabiki. Tuungane kwa pamoja kutetea haki za Taifa,” alisema Mbatia ambaye ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vinne vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.

Aliwataka wabunge wenzake kujifunza kutoka nchi ambazo zilijaribu kuendesha vita hiyo, akitoa mfano wa Zimbabwe ambayo ilishindwa na matokeo yake kuua uchumi wake baada ya ushabiki wa kisiasa kuingizwa na kusababisha mambo kuharibika tofauti na matarajio yaliyokuwapo.

Kuepuka hayo, Mbatia alisema mchakato wa kuandika Katiba mpya itakayoweka misingi imara ya kulinda rasilimali badala ya kutegemea mtu mmoja, hauepukiki.

“Katiba mpya haiepukiki. Leo yupo Rais Magufuli kesho atakuja mwingine. Katiba itasaidia kusimamia uchumi wetu,” alisema mwenyekiti huyo wa NCCR-Mageuzi

Wakati mjadala wa kupitisha azimio la kumpongeza Rais, Mwanasheria Mkuu wa Chadema na mbunge wa Iramba Mashariki, Tundu Lissu alisema tahadhari inahitajika kushughulikia suala la makinikia kwa kuwa taarifa za kamati zote mbili hazina kitu cha maana.

Alipendekeza kuwa ili kujadili suala hilo kwa mapana, iwepo semina kwa wabunge wote ili kuwajengea uwezo wa kuchangia kwa namna itakayoongeza tija hata kutambua upungufu uliopo katika ripoti za kamati zilizoundwa na Rais.

Siku moja kabla mkurugenzi mtendaji wa Barrick Gold Corporation inayomiliki asilimia 64 za Acacia kuonana na Rais Magufuli, Lissu aliziita ripoti hizo kuwa ni: “Professorial rubbish (upuuzi wa kisomi).”