Sababu Polepole, Kalanga kukutana usiku hii hapa

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole 

Muktasari:

Polepole na Kalanga kwa pamoja, walizungumza na Watanzania usiku wa kuamkia leo kupitia kurasa za mtandao wa kijamii za facebook na Twitter za katibu huyo wa itikadi na uenezi


Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ametoa sababu za mkutano wa kumkaribisha aliyekuwa mbunge wa Monduli (Chadema), Julius Kalanga kufanyika usiku.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumanne Julai 31, 2018 Polepole amesema mkutano huo umefanyika jana usiku kwa kuwa ndio muda pekee uliopatikana kutokana na kutingwa na shughuli nyingi.

Polepole na Kalanga kwa pamoja, walizungumza na Watanzania usiku wa kuamkia leo kupitia kurasa za mtandao wa kijamii za facebook na Twitter za katibu huyo wa itikadi na uenezi.

Katika mazungumzo hayo, Kalanga alitangaza kujivua uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM, usiku huohuo.

Soma Zaidi:

“Unajua jana nilikuwa Tarime (Mara), nikaenda Mwanza pale nilikuwa na kikao, kisha nikaenda Dar es Salaam  ambako nilikuwa na shughuli. Baadaye nilikwenda  Kilimanjaro na Arusha. Nilifanya mkutano jana usiku kwa kuwa ndio muda niliokuwa nao,” amesema Polepole.

“Ingawa ilikuwa usiku lakini mazungumzo yale yamefuatiliwa na watu wengi kweli kweli na wengi walipiga simu hadi kutoka nje ya nchi.”

Amesema kuna wabunge zaidi wa Chadema wanatamani kujiunga na CCM.

“Kuna wabunge ambao tumeweka msimamo kama chama kwamba hatuwezi kuwapokea hata wakitaka. Huwezi kuwa na mbunge yeye kazi yake ni kuota ndoto tu,” amesema.