Safari ya Tz ya viwanda yaanza

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.

Muktasari:

Akizungumza na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka China, Mwijage alisema mwanzo kiwanda hicho kitatumia malighafi kutoka nje lakini baadaye kitatumia inayopatikana nchini kutoka Liganga wilayani Ludewa.

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema kiwanda cha chuma kinachojengwa Mlandizi mkoani Pwani kitazalisha bidhaa hiyo kwa kutumia malighafi inayopatikana nchini.

Akizungumza na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka China, Mwijage alisema mwanzo kiwanda hicho kitatumia malighafi kutoka nje lakini baadaye kitatumia inayopatikana nchini kutoka Liganga wilayani Ludewa.

Mwijage alisema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, upatikanaji ajira na kufanikisha azma ya Serikali kuifanya Tanzania nchi ya viwanda.

Alisema awamu ya kwanza ya kiwanda hicho kinachomilikiwa na Mtanzania kwa ubia na wawekezaji wa China, utakamilika mwaka huu na kufunguliwa na Rais John Magufuli. Mwijage alisema uwapo wake Mlandizi utaboresha hali ya uchumi kwa wakazi wa eneo hilo na Taifa.

Alisema Serikali inatarajia kukusanya kodi ya Sh200 bilioni kwa mwaka na kuajiri zaidi wafanyakazi 500 na kwamba, kiwanda kingine cha vigae kinajengwa wilayani Mkuranga ambacho kitakamilika mwaka huu.

Mwijage aliueleza wajumbe huo kwamba Serikali itawapatia wawekezaji wa Kichina eka 700, ili wajenge kiwanda kikubwa cha nguo.

Naibu Waziri wa Biashara wa China, Qian Keming alisema viwanda vitakavyojengwa nchini vitatoa ajira kwa Watanzania.

“Urafiki wetu utaendelea kudumishwa kwa kuwekeza katika maeneo mbalimbali kadri fursa zitakapokuwa zikijitokeza,” alisema Keming.

Keming alisema uwekezaji huo unasukumwa zaidi na uhusiano wa karibu kati ya nchi hizo mbili, ambao uliasisiwa na aliyekuwa Rais wa China, hayati Mao Tse-tung na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere. Alisema Serikali yake inafurahishwa namna Tanzania ilivyojiwekea mkakati wa kufufua uchumi wa viwanda.