Sahara Energy yachangia vitabu 2000 Pugu Sekondari

Kaimu Kamishna wa Elimu, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi,  Nicolas Buretta  akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Pugu, iliyoko jijini Dar es Salaam baada ya kuzindua maktaba ya shule iliyokarabatiwa na kuwekwa vitabu na Sahara Foundation  Tanzania hafla iliyofanyika mwishoni mwa juma.Picha na Emanuel Herman

Muktasari:

Mbali na kuchangia vitabu hivyo, kampuni hiyo  pia imefanya maboresho katika maktaba ya shule hiyo ambayo aliwahi kufundisha Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Dar es Salaam. Katika kuendeleleza juhudi za kutekeleza  sera ya elimu bure chini ya Serikali ya Awamu ya Tano, Kampuni ya Sahara Energy imechangia vitabu 2000 kwa Shule ya Sekondari Pugu.

Mbali na kuchangia vitabu hivyo, kampuni hiyo  pia imefanya maboresho katika maktaba ya shule hiyo ambayo aliwahi kufundisha Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vitabu hivyo, Meneja wa huduma kwa jamii wa Sahara Energy, Babatomiwa Adesida amesema mchango huo unalenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.

Mkuu wa kitengo cha  mawasaliano wa kampuni hiyo, Bethel Obioma amesema anaamini  mchango huo utasaidi kutoa maarifa kwa vijana ambao watakuwa viongozi bora wa Taifa hili hapo baadae kwa sababu shule hiyo ina historia hiyo.

Mkuu wa shule hiyo, Juvenus Mutabuzi amesema maboresho ya maktaba pamoja na vitabu hivyo vitakuwa msaada mkubwa hasa kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita ambao wamepata vitabu vipya 1000, ambavyo walikuwa wanavisubiri kutoka serikalini.