Serikali: Mali za Mbicu zakabidhiwa Mbifacu

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha 

Muktasari:

Baada ya kuelemewa na madeni na kuyumba kwa soko la kahawa, Mbicu ilikabidhiwa kwa mfilisi mwaka 1994/95 kabla haijafutwa kwenye daftari la Serikali kisha kufilisiwa.

Dodoma. Baada ya kufilisika kwa Mbinga Cooperative Union (Mbicu) kutokana na kuelemewa na madeni, mali zake zimekabidhiwa kwa Mbinga Farmers Cooperative Union (Mbifacu) inayoendelea kulipa madeni yaliyobaki.

Baada ya kuelemewa na madeni na kuyumba kwa soko la kahawa, Mbicu ilikabidhiwa kwa mfilisi mwaka 1994/95 kabla haijafutwa kwenye daftari la Serikali kisha kufilisiwa.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha amesema mwaka 2007 baada ya kuanzishwa kwa Mbifacu, wanachama walikubali kulipa deni la Sh155 milioni kutoka Golden Impex lililokamilishwa Machi 2013.

"Baada ya kulipa deni hilo, Mbifacu ilikabidhiwa asilimia 70 ya mali za Mbicu na kuanza kuzisimamia. Sehemu iliyobaki itakabidhiwa baada ya kusainiwa kwa mkataba wa maridhiano (MoU) baina ya mfilisi na Mbifacu," amesema Ole Nasha.

Wakati inafilisiwa, Mbicu ilikuwa inadaiwa zaidi ya Sh2.1 bilioni ilhali mali zake zilikuwa ni Sh752.8 milioni.

Kutokana na kuyumba kwa vyama vingi vya ushirika, waziri huyo alimfahamisha Mbunge wa Mbinga Vijijini, Martin Msuha aliyetaka kufahamu mchango wa Serikali kwenye suala hilo.

Msuha alitaka kufahamu kama Serikali ipo tayari kulipa deni la wakulima la Sh424 milioni lililoachwa na Mbicu.

"Mpaka sasa Mbifacu imelipa Sh36 milioni ya deni la watumishi wa Mbicu kutoka kwenye ziada iliyopatikana na wanaendelea kulipa madeni mengine yaliyobaki," amesisitiza ole Nasha.