Serikali kuhakiki upya meli zote zilizosajiliwa Tanzania Bara, Z’bar


Muktasari:

        Makamu wa Rais amesema kamati maalumu imeundwa kuchunguza mchakato wa usajili unavyokuwa na zilizokwisha sajiliwa zinavyofanya kazi.

Serikali imeunda kamati maalumu itakayoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama itakayofanya mapitio ya meli zote zilizosajiliwa na zitakiazosajiliwa nchini ili kuangalia mwenendo wake.

Hatua hiyo ya Serikali inakuja kipindi ambacho meli mbili zilizosajiliwa nchini zimekamatwa ughaibuni zikisafirisha dawa za kulevya na silaha.

Meli hizo ni Kaluba yenye usajili namba IMO 6828753 iliyomatwa maeneo ya Jamhuri ya Dominican Desemba 27, 2017 ikiwa na wastani wa kilo 1,600 za dawa za kulevya na Andromeda yenye usajili IMO 7614666 iliyokamatwa ikisafirisha silaha kinyume cha sheria za kimataifa.

Jana, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam alisema kuundwa kwa kamati hiyo kunalenga kufahamu kwa kina mchakato wa usajili wa meli unavyokuwa na zilizokwisha sajiliwa zinavyofanya kazi.

Alisema kutokana na meli hizo kukiuka kiapo walichosaini cha kutokujihusisha na biashara za silaha, dawa za kulevya na binadamu, zimefutiwa kibali na kuagiza zishushe haraka bendera ya Tanzania na wakati zikiendelea kupambana na tatizo lao.

Makamu wa Rais alisema baada ya kutokea kwa tatizo hilo, Rais John Magufuli aliagiza kuitishwa kikao cha dharura baina ya viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambacho kilifanyika juzi Zanzibar.

Alisema katika kikao hicho, Zanzibar iliwakilishwa na makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idi na ndicho kilichokubaliana kuundwa kwa kamati hiyo.

“Kwa kuwa uendeshaji wa biashara hii unaonekana kuleta utata na kutia dosari kubwa Taifa letu na kuharibu sifa njema za nchi zetu, imeonekana haja ya kuunda kamati ya pamoja ya wataalamu wa Serikali ya Tanzania na Zanzibar ikishirikisha vyombo vya ulinzi na usalama,” alisema Samia na kuongeza;

“Kamati hiyo itapitia upya usajili uliokwishafanyika na kuzihakiki taarifa za meli zote zilizosajiliwa nchini mwetu, kuangalia mwenendo mzima wa usajili na hatimaye kutoa mapendekezo na ushauri kwa Serikali.”

Alisema kuanzia sasa, kabla ya meli kupewa usajili kutafanyika utaratibu wa kuzichunguza kwa kina pamoja na wamiliki wake kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya Serikali vikiwamo vile vya ulinzi na usalama.

Makamu wa Rais alisema jukumu lingine la kamati hiyo ni, “Kufanya mapitio ya sheria zetu ili kuzipa nguvu zaidi taasisi zinazosimamia usajili wa meli. Wakati wa mapitio ya sheria, timu ya wataalamu itaangalia kwa makini kodi zinazotozwa na mchango wake nchini ili zisiwe kivutio kwa meli zisizokidhi viwango kuomba usajili Tanzania.”

Alisema wataendelea kushirikiana na nchi nyingine kwa kuzipa ruhusa kukamata na kuzipekua meli zinazopeperusha bendera ya Tanzania wakati wote zinapohisiwa kuwa zinafanya uhalifu au masuala ambayo hayaruhusiwi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zinazokubalika kimataifa na wakati wa usajili.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira, Janauri Makamba alisema Serikali haihusiki na biashara au makosa yaliyofanywa na wamiliki wa meli hizo na kinachopiganiwa na Tanzania ni bendera yake kutumika vibaya kwani wanashusha hadhi, sifa na heshima ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini Zanzibar, Abdallah Kombo alisema hadi kufikia Desemba mwaka jana meli 457 za nje zilikuwa zimesajiliwa na 61 za ndani huku msajili wa meli kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Kapteni Mussa Mandia akisema ofisi yake imesajili meli 88.