Tuesday, February 14, 2017

Serikali yavuna Sh466 milioni mnada wa Tanzanite

 

By Mussa Juma, Mwananchi

Arusha. Serikali imepata kodi ya Sh466.4 kutokana na mauzo ya Sh9.3 bilioni ya madini ya Tanzanite kupitia mnada uliofanyika mjini Arusha.

Akizungumza katika mnada huo, Mkurugenzi wa Uthaminishaji wa Almasi na Vito Wizara ya Nishati na Madini (Tansolt), Archard Karugendo amesema katika mauzo hayo, Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro imepata Sh27.9 milioni.

Karugendo amesema katika mnada huo wa pili kufanyika nchini, Kampuni ya TanzaniteOne inayomilikiwa kwa ubia kati ya Sky Associate na Stamico, ndiyo iliongoza kwa kuuza madini na kupata Sh8.8 bilioni.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendela amesema licha ya madini hayo kuwa ni ya Taifa, ni muhimu wakazi wa Wilaya ya Simanjiro waone matunda yake.

Bendera amesema ni aibu Tanzanite inatoka Simanjiro, lakini wilaya hiyo ndiyo ya mwisho kwa elimu mkoani Manyara na kuwapo kwa shida kubwa ya maji, huduma za afya na Mererani inaongoza kwa maambukizi ya HIV ambayo yamefikia asilimia 18.

Wakizungumza baada ya mnada huo, wakurugenzi wa TanzaniteOne, Faisal Shabhai na Hussein Gonga wameeleza kuridhishwa na  kuahidi kuendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha wanauza madini katika minada nchini.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe amesema wizara hiyo, itaendelea kuwezesha minada ili kuhakikisha wanunuzi wakubwa wa madini wanafika nchini kununua madini katika masoko yanayotambulika kisheria.

 

-->