Sh10 milioni za wabunge CCM mikononi mwa Takukuru

Muktasari:

Takukuru imeanza kuchunguza tuhuma hizo siku chache baada ya Mbowe kuziibua alipokuwa akimuuliza swali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, bungeni mjini Dodoma.

Dar es Salaam. Baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), Freeman Mbowe kuibua tuhuma dhidi ya wabunge wa CCM akidai wamepewa Sh10 milioni kila mmoja ili wapitishe mpango wa maendeleo ya Taifa na muswada wa Sheria za Huduma za Habari, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa imeanza uchunguzi.

 

Takukuru imeanza kuchunguza tuhuma hizo siku chache baada ya Mbowe kuziibua alipokuwa akimuuliza swali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, bungeni mjini Dodoma.

 

Hata hivyo, swali hilo halikujibiwa na Waziri Mkuu baada ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kumkingia kifua akidai swali hilo halikuwa la kisera.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola amesema wameanza kufanya uchunguzi juu ya suala hilo kwa sababu ni jukumu lao na watalifanya kiuhakika.

 

 “Kama Rais amesema tunachunguza suala hilo mnataka mimi niseme nini? Ndiyo, tumeanza kuchunguza, Takukuru ni chombo chake na tumeanza kazi hiyo. Kama na wewe una ushahidi tuletee tuufanyie kazi,” amesema Mlowola alipokuwa akijibu swali aliloulizwa na mwandishi wetu juu ya suala hilo.

 

Alipoulizwa kama analifanyia kazi suala hilo, Kamishna Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda amesema Takukuru ndiyo wenye kazi hiyo kwa sasa.

 

Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala amesema Takukuru inatakiwa kuzifanyia kazi tuhuma hizo kwa sababu ni rushwa kama yalivyo matukio mengine ya rushwa.