Shahidi asimulia alivyomkamata Lissu nyumbani

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu 

Muktasari:

Mgonja anayetoka Kituo cha Polisi Wazo Hill, ni shahidi wa upande wa mashtaka ambaye aliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa, alidai jana kuwa Juni 6, mwaka jana, alipewa maelekezo ya kumkamata Lissu na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO), Camilius Wambura.

Dar es Salaam. Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kawe, Yustino Mgonja ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi alivyomkamata Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu nyumbani kwake Tegeta Kibaoni.

Mgonja anayetoka Kituo cha Polisi Wazo Hill, ni shahidi wa upande wa mashtaka ambaye aliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa, alidai jana kuwa Juni 6, mwaka jana, alipewa maelekezo ya kumkamata Lissu na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO), Camilius Wambura.

Alidai kuwa siku hiyo baada ya kupatiwa maelekezo, alienda nyumbani kwa Lissu, Tegeta Kibaoni saa tatu usiku ili kumkamata na kwamba, alimsaka lakini hakumpata.

Shahidi huyo alidai Juni 29, mwaka jana, alienda tena nyumbani kwa Lissu saa saba kasoro mchana, ambako alimkamata na kumpeleka kwa ZCO.

Baada ya ushahidi huo, kesi iliahirishwa hadi Julai 10 itakapoendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na kesi ya uchochezi akidaiwa Juni 28, mwaka jana, akiwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alitoa kauli za uchochezi kuwa:

“Mamlaka ya Serikali mbovu ni ya kidikteta uchwara inahitaji kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote. Huyu dikteta uchwara lazima apingwe kila sehemu.

“Kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga, nchi inaingia ndani ya giza nene.’’