Sheikh ataka wanaombeza JPM walaaniwe

Muktasari:

  • Sheikh Mwansasu ametoa kauli hiyo jana (Jumatatu) usiku alipokuwa akisoma dua ya kumuombea  Rais Magufuli kwenye kusanyiko la waumini wa Kiislamu wa mikoa ya Mbeya na Songwe.
  • Dua hiyo ilienda sambamba na  futari iliyoandaliwa na Taasisi ya Tulia Trust, kwa waumini wa dini ya Kiislam na kufanyikia katika Ukumbi wa Royal Tughimbe jijini hapa.

Mbeya. Sheikh   wa  Mkoa  wa  Mbeya,  Mohamed  Mwansansu  amesema anayezibeza  juhudi za  Rais John Magufuli anapaswa kulaaniwa.
Sheikh Mwansasu ametoa kauli hiyo jana (Jumatatu) usiku alipokuwa akisoma dua ya kumuombea  Rais Magufuli kwenye kusanyiko la waumini wa Kiislamu wa mikoa ya Mbeya na Songwe.

Dua hiyo ilienda sambamba na  futari iliyoandaliwa na Taasisi ya Tulia Trust, kwa waumini wa dini ya Kiislam na kufanyikia katika Ukumbi wa Royal Tughimbe jijini hapa.
“Lazima kwa umoja wetu tuendelee kuungana na Rais wetu katika kupambana na wezi na mafisadi wa rasilimali zetu, na nitamshangaa mtu mwenye akili timamu anapinga juhudi hizi kwa sababu ya itikadi za chama chake  au mtu yeyote ni lazima aangamie mara moja,” amesema.
Amesema anachokifanya Rais Magufuli ni kwa  ajili ya masilahi ya Watanzania wote na siyo familia yake wala chama chake hivyo Watanzania kwa umoja wao wanapaswa kuungana  kwa pamoja katika kumuunga mkono ikiwa ni pamoja na kumuombea kwa Mungu kwani ndiye mlinzi mkuu.
Kuhusu futari hiyo amesema alichokifanya Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Dk Tulia Ackson kupitia taasisi yake  ni jambo la  thawabu hasa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani wakati yeye ni Mkristo.
“Huu ni mfano mkubwa, Tulia kuwapa chakula Waislamu hivyo na sisi waislamu tuweze kufanya hivi kwa kuwaita jamii isiyo ya kiislamu na kukaa nayo pamoja zungumza na kufuturu pamoja,”amesema.
Kaimu Sheikh  wa Mkoa wa Songwe,  Hussein Issah Batuzi, amesema uislamu ni kuitisha jamii tofauti tofauti kukaa pamoja na kuzungumza na kuleta amani  na utulivu badala ya kuleta shida, vurugu na patashika kwa jamii nyingine jambo ambalo mwenyezi Mungu anakataa.
Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi  Mkoa wa Mbeya (CCM) Wilson Nkhambaku, ametoa rai kwa viongozi hao wa dini ya kiislamu na Watanzania wote bila kujali tofaui za kiitikadi kuendelea kuwaombea viongozi wa Serikali kwa kazi ngumu wanayofanya ya kupambana na mafisadi wa rasilimali za Taifa.
“Naomba muendelee kuwaombea vingozi wetu ili Mungu aweze kuwapa ujasiri mkubwa na upendo kwa manufaa ya Taifa letu na waendelee kusimamia uchumi wa nchi yetu kwani kufanya hayo kunahitaji ujasiri na ulinzi wa mwenyezi Mungu.”amesema.