Simulizi ya ndugu, jamaa saa chache baada ya ajali

Waokoaji wakijipanga kuwaokoa majeruhi wa ajali ya kivuko cha Mv Nyerere kilichozama wilayani Ukerewe juzi. Picha na mtandao

Muktasari:

Mbali ya mchumba huyo, kwa nyakati tofauti, ndugu hao walizungumza jana kwa simu na waandishi wa Mwananchi na kueleza jinsi ajali hiyo iliyotokea juzi mchana katika Ziwa Victoria ilivyowaachia simanzi miongoni mwao kwani walipoteza ndugu watatu wa familia moja huku baadhi wakipoteza ndugu sita.

Dar es Salaam. Wakati Maulid Mussa (49) mkazi wa Ukerewe mkoani Mwanza akieleza alichozungumza na rafiki yake saa chache kabla ya kufariki dunia baada ya kivuko cha Mv Nyerere kuzama, ndugu wa Phinias Turumanya wameeleza jinsi mwenzao alivyompoteza mchumba wake, aliyekuwa akimpeleka kumtambulisha kwa wazazi.

Mbali ya mchumba huyo, kwa nyakati tofauti, ndugu hao walizungumza jana kwa simu na waandishi wa Mwananchi na kueleza jinsi ajali hiyo iliyotokea juzi mchana katika Ziwa Victoria ilivyowaachia simanzi miongoni mwao kwani walipoteza ndugu watatu wa familia moja huku baadhi wakipoteza ndugu sita.

Hadi jana saa 10:16 jioni, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema miili ya watu 126 ilikuwa imeopolewa na ilipofika saa 12:00 jioni miili hiyo ilifika 131.

Kivuko hicho kilichokuwa kikitokea Kisiwa cha Bugolora wilayani Ukerewe kuelekea Kisiwa cha Ukara, kilizama mita 50 kabla ya kutia nanga huku ikielezwa kuwa kilikuwa na abiria wengi ambao idadi yao haikupatikana.

Katika maelezo yake, Mussa alisema alinusurika baada ya kukatisha safari yake aliyokuwa amepanga kuifanya juzi kwa kutumia kivuko hicho.

Katika safari hiyo, ilikuwa aongozane na rafiki yake aliyemtaja kwa jina moja la Joseph ambaye alilazimika kwenda peke yake hivyo kubaki wakiwasiliana kwa simu.

“Ningekuwa miongoni mwa waliopata ajali kwa kuwa ilikuwa nipande kivuko kile ila kutokana na msongomano wa watu na mzigo ulikuwamo niliamua kuahirisha safari,” alisema.

Mussa ambaye ni mvuvi, alisema aliwasiliana na Joseph wakati kivuko hicho kilipopata hitilafu na alimueleza kuwa kinakaribia kuzama.

“Alinipigia simu na kunieleza kuwa kuna matatizo na kwamba walikuwa wanakaribia kuzama. Nilimuuliza tatizo ni nini? Akanijibu kuwa ajali imeshatokea na kwamba abiria walikuwa wamelemea upande mmoja wa kivuko na kusisitiza kuwa muda huo ndio chombo kilikuwa kikizama,” alisema Mussa na kuongeza kwamba baada ya muda mawasiliano na rafiki yake huyo yalikatika.

Alisema baada ya hapo, alitafuta njia ya kufika eneo la tukio lakini haikuwezekana kwa kuwa hakukuwa na kivuko kingine.

“Tulichukua usafiri kuelekea kwenye eneo la tukio lakini hatukufanikiwa kufika upande wa pili na hata mawasiliano yalikata,” alisema Mussa na kubainisha kuwa jana alipata taarifa kuwa Joseph alifariki dunia.

Akizungumzia ndugu yake kupoteza mchumba katika ajali hiyo, dada wa Phinias mkazi wa Kijiji cha Bukiko huko Ukara, Stella Masondore alisema kaka yake anayeishi Ukerewe, juzi alikuwa katika kivuko hicho akienda kumtambulisha mchumba wake kwa wazazi.

“Akiwa njiani kivuko kilizama na mchumba wake amefariki dunia lakini yeye (Phinias) aliokolewa akiwa hai na sasa yupo hospitali na hali yake ni nzuri,” alisema Stella.

Alisema mbali na kumpoteza wifi yao katika ajali hiyo, pia wamepoteza ndugu watatu ambao aliwataja kuwa ni Turumanya Mtware, Veronica Turumanya na Tudesiana Bwire.

Aidha, familia ya Magessa Mrapirapi imepoteza ndugu sita wa familia moja waliokuwa wakiishi Kijiji cha Bwisha, Ukara ambao walikuwa wakirejea kutoka kwenye gulio.

Akizungumza na Mwananchi, Mtabi Magessa aliwataja ndugu hao waliofariki dunia kuwa ni Gabaseki Magessa, Siwema Magessa, Nyambhoi Magessa, Siwema Magessa, Nyabhori Donart na Nyambori Maero.

Madaraka Mganga ambaye mama yake mzazi, Gabaseki amefariki dunia katika ajali hiyo, alisema kabla ya janga hilo, alikuwa akifanya biashara ya kuuza sabuni na alikuwa amekwenda kwenye gulio Bugolora.