Sintofahamu kuhojiwa polisi kwa Mchungaji KKKT

Muktasari:

  • Taarifa za kuchukuliwa na polisi ofisini kwake mchungaji huyo zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii juzi usiku.

Dar/Moshi. Tukio la kukamatwa kwa mchungaji kiongozi wa Usharika wa Karanga wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Fred Njama limeibua sintofahamu.

Taarifa za kuchukuliwa na polisi ofisini kwake mchungaji huyo zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii juzi usiku.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, polisi walimchukua mchungaji huyo juzi ofisini kwake na kumpeleka hadi katika kiwanda alipochapa kitabu cha hotuba yake aliyoitoa Machi 10 katika Kanisa la Usharika wa Karanga.

Wakati akiwasilisha taarifa yake katika Mkutano Mkuu wa 21 wa usharika huo siku hiyo, Mchungaji Njama alitaja mambo sita aliyodai yanaitafuna nchi.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk Martin Shao.

Habari za ndani zinasema kuwa juzi jioni maofisa wa polisi walifika katika usharika huo uliopo eneo la Soweto mjini Moshi na kufanya upekuzi na kuchukua laptop na flash ya Mchungaji Njama.

Habari hizo zinasema baada ya kuchukua vitabu vilivyokuwa vimebaki kiwandani na kuchukua vingine vilivyokuwa kanisani, polisi hao walimchukua Mchungaji Njama na kwenda kumhoji hadi saa nne usiku kabla ya kuachiwa kwa dhamana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alipoulizwa na Mwananchi jana alisema suala hilo lilishughulikiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Moshi.

“Suala hilo limeshughulikiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na mimi bado halijanifikia ili niwe katika nafasi nzuri ya kulizungumzia,”alisema.

Mwananchi lilimtafuta mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Moshi, Kippi Warioba ambaye alisema, “Suala hilo siwezi kulizungumzia katika simu”.

Kippi, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Moshi alimtaka mwandishi wetu kufika ofisini kwake ili wazungumze ana kwa ana, lakini mwandishi alipokwenda ofisi hizo saa 6:00 mchana aliambiwa mkuu huyo wa wilaya hajafika tangu asubuhi.

Taarifa zilizolifikia Mwananchi jana jioni zinaeleza kuwa Mchungaji Njama aliachiwa juzi saa 4 usiku na kwamba alikuwa ameongozana na mawakili wawili binafsi, wakili wa dayosisi na mchungaji mmoja.

Taarifa hizo zinasema kuwa polisi wanaishikilia simu yake na vifaa vingine kama kompyuta mpakato (laptop) na flash.

Alipoulizwa kuhusu tukia hilo, Mkuu wa KKKT, Frederick Shoo alisema, “Kwa sasa sina la kuzungumza kwani niko nje ya Mkoa wa Kilimanjaro, lakini tunafuatilia kujua kwa nini alikamatwa na alifanya uhalifu gani.”

Machi 10 mwaka huu, Mchungaji Njama alitaja mambo sita aliyodai yanaitafuna nchi wakati akiwasilisha taarifa yake katika Mkutano Mkuu wa 21 wa usharika huo.

Mchungaji Njama, ambaye pia ni mkuu wa pili wa Jimbo la Kilimanjaro Kati alitaja mambo hayo kuwa ni pamoja na hali ya uchumi, ajira kwa vijana, ughali wa matibabu na tangazo la elimu bure.

Njama, ambaye pia ni mchungaji kiongozi wa Usharika wa Karanga mjini Moshi, alitaja mambo mengine kuwa ni hali ya kisiasa nchini na kundi kubwa la wastaafu kutolipwa mafao yao.

Mkutano huo mbali na kuhudhuriwa na Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Kati, Mchungaji Kennedy Kisanga na wachungaji wa sharika jirani, ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka jumuiya 32.

Hata hivyo, kuhojiwa kwa mchungaji huyo kumeibua hisia miongoni mwa waumini na jamii kwa ujumla.

Wakili wa kujitegemea wa jijini Dar es Salaam, Frank Mushi alisema kukamata watu wanaotumia haki yao ya kikatiba kutoa maoni yao, kunaichafua taswira nzuri ya Tanzania kimataifa. “Katiba inamruhusu na inampa kila mtu haki ya kushiriki katika shughuli za Serikali yake. Ikitokea alichokisema sio ukweli anapaswa kuelezwa ukweli ni upi sio kukamatwa,” alisema Mushi.

“Serikali itawajibika kwa wananchi, sasa kama mwananchi anasema kuna shida, Serikali inatakiwa iseme hiki anachokisema sio sawa ila ukweli ni huu. Kutofautiana kimtizamo sio kosa” alisisitiza.

Wakili huyo alitolea mfano wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, aliyewahi kusema mtu akisema Serikali haijafanya chochote, Serikali inapaswa kuwaonyesha barabara, shule na hospitali.

Kuhojiwa kwa Mchungaji Njama si tukio la kwanza kuwapata viongozi wa dini hapa nchini katika miezi ya hivi karibuni.

Januari mwaka huu, maofisa wa Idara ya Uhamiaji walimwita Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge, wilayani Ngara, Severine Niwemugizi (62), na kumhoji kuhusu uraia wake.

Kuhojiwa kwake kulikuja miezi michache baada ya askofu huyo kutamka kwamba yuko tayari kuitwa mchochezi endapo kuungana na wanaharakati wengine kudai katiba mpya kutachukuliwa hivyo.

Pia, mwezi Januari, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe, alihojiwa na kupekuliwa kwa zaidi ya saa sita na maofisa ya Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa kile walichoeleza ni kufuatilia ulipaji kodi wake.

Hatua hiyo ilikuja siku chache baada ya Askofu Kakobe kutamka katika ibada ya mkesha wa Krismasi Desemba mwaka jana kuwa ana fedha nyingi kuliko Serikali.