Siri nzito yatawala Kamati Kuu CCM

Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli akiagana na wajumbe wa Kamati Kuu baada ya kikao kilichofanyika jijini Dar es salaam jana. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • CCM imeanza mchakato wa uchaguzi wa viongozi wake kuanzia ngazi ya shina na sasa umefikia wilayani ambako majina ya wagombea yanachujwa na vikao vya juu ambavyo vinafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia jana hadi mwishoni mwa wiki.

Dar es Salaam. Kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilianza jana chini ya Mwenyekiti wake, John Magufuli, lakini haikuweza kufahamika mara moja uamuzi uliofikiwa katika kuchuja majina ya wagombea wa nafasi za uongozi katika ngazi ya wilaya.

CCM imeanza mchakato wa uchaguzi wa viongozi wake kuanzia ngazi ya shina na sasa umefikia wilayani ambako majina ya wagombea yanachujwa na vikao vya juu ambavyo vinafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia jana hadi mwishoni mwa wiki.

Baada ya Kamati Kuu kumaliza vikao vyake vya siku mbili leo, CCM itakuwa na kikao cha Halmashauri Kuu ambayo itabariki mapendekezo ya chombo hicho cha utendaji cha chama hicho tawala.

Hakuna taarifa zilizotolewa jana kuhusu maazimio ya kikao hicho na juhudi za gazeti hili kupata wahusika ziligonga mwamba.

Matokeo yake, usiri huo uliibua ubashiri ulioenezwa katika mitandao ya kijamii kuwa wabunge wachache ambao wamekuwa wakionekana kuikosoa Serikali, wamevuliwa uanachama.

Hata hivyo, gazeti hili halikuweza kuthibitisha habari hizo.

Picha zilizotumwa na Ikulu jana zinaonyesha wajumbe wa kamati hiyo wakiwa wamesimama kabla ya kuanza kikao, bila ya kuwapo katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Picha moja inamuonyesha Rais Magufuli akiingia kikaoni, akiwa ameongozana na naibu katibu mkuu wa CCM-Bara, Rodrick Mpogolo ambaye anaonekana kuwa ndiye aliyeshika nafasi ya Kinana.

Mpogolo pia anaonekana pembeni ya Magufuli ndani ya kikao kuthibitisha kuwa alishika nafasi ya Kinana sehemu fulani ya kikao hicho.

Hakuna taarifa zilizotolewa kuhusu kutokuwepo kwa mtendaji huyo mkuu wa CCM na kama aliingia kikaoni baadaye.

Picha nyingine inamuonyesha Waziri Mkuu wa zamani, Salim Ahmed Salim, ambaye huenda alikaribishwa kuhudhuria kikao hicho.

Salim na marais wa awamu tatu zilizotangulia kabla ya Serikali ya Jakaya Kikwete, ndiyo waliofanya kazi kubwa ya kutuliza wajumbe wa Halmashauri Kuu mwaka 2015 wakati zogo lilipoibuka kutokana na jina la Edward Lowassa kuenguliwa na Kamati Kuu kuwania kugombea urais kwa tiketi ya CCM.

Habari ambazo Mwananchi ilizipata jana zinaeleza kuwa Kamati Kuu ilianza kwa kupokea taarifa ya Kamati ya Maadili kuhusu mwenendo wa wagombea wakati wa mchakato wa kuchukua fomu hadi sasa.

Taarifa hiyo ndiyo inayotumiwa na Kamati Kuu kupitisha au kuondoa wagombea, ambao hawakuruhusiwa kujitangaza, kujipitisha kwa wapigakura wala kutumia mbinu nyingine yoyote kutafuta kura hadi watakapotambulishwa mbele ya wapigakura.

Pia ripoti hiyo itawaweka bayana wanachama ambao wamesukumwa na watu wenye fedha ili wawatumie kwa malengo binafsi baadaye.

Pia, taarifa zinasema mchujo huo utawagusa wale waliotahadharishwa kugombea kutokana na vitendo vyao vya ukuikwaji wa maadili ndani ya chama.

Taarifa zinaeleza kuwa licha ya kuweka miiko ya kugombea uongozi ndani ya chama, kama kuwakataza watumishi wa Serikali kugombea nafasi ambazo baadaye zitawalazimu kusimama kwenye majukwaa ya kisiasa kunadi sera za chama, bado baadhi walijitokeza kugombea na kupitishwa na vikao vya ngazi za chini.

Kikao hicho pia kinaangalia maadili ya walioomba kugombea ili kuepuka kupitisha wagombea ambao ni watuhumiwa wa ubadhirifu wa mali za chama, wasio wakazi wa maeneo husika na waliopitishwa baada ya wengine kuonewa katika uteuzi na kuwapo mgombea mmoja pekee aliyepitishwa badala kuwa na ushindani.