Songombingo zaanza Soko la Sido Mbeya

Wafanyabiashara wakifanya usafi katika sehemu vilipokuwa vibanda vyao vya biashara kwenye soko la Sido lililoteketea kwa moto jijini Mbeya.Picha Picha na Godfrey Kahango.

Muktasari:

Hali hiyo imeibuka baada ya wafanyabiashara hao kuanza ujenzi wa vibanda vya kudumu jambo ambalo lilizuiwa na Serikali.

Mbeya. Mvutano mkubwa umeibuka baina ya Serikali na wafanyabiashara wa Soko la Sido Mwanjelwa jijini hapa ambalo usiku wa kuamkia juzi lilikumbwa na moto.

Hali hiyo imeibuka baada ya wafanyabiashara hao kuanza ujenzi wa vibanda vya kudumu jambo ambalo lilizuiwa na Serikali.

Juzi, uongozi wa mkoa kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika ulitoa taarifa ya kuundwa kwa kamati maalumu ya kuchunguza na kufanya tathmini ya hasara iliyotokana na chanzo cha moto huo iliyopewa siku tano na kuwataka viongozi wa soko hilo kuwaambia wafanyabiashara hao wasianze ujenzi wa vibanda vingine hadi litakapotolewa tamko rasmi.

Lakini jana asubuhi, katibu wa soko hilo, Alanus Ngogo alisema walishindwa kutii agizo hilo la kwenda kuwaambia wafanyabiashara wasiendelee na ujenzi wa vibanda vyao na kumtaka Ntinika kwenda mwenyewe pamoja na vyombo vyake ya ulinzi na usalama kuzungumza na wafanyabiashara hao.

“Jana walitukubalia kwamba leo (jana) saa nne asubuhi, mkuu wa wilaya anakuja kuzungumza na wafanyabiashara hawa, maana tuliona sisi viongozi hawatatuelewa hiki walichotuagiza. Lakini hawa watu wana njaa na manung’uniko hivyo wameamua kuanza ujenzi wa vibanda vya kudumu bila hata ya kusubiri kauli mbadala ya Serikali,” alisema katibu huyo.

Wakiwa na matumaini ya kumuona mkuu huyo wa wilaya, wafanyabiashara hao walisubiri kwa muda mrefu kama walivyoahidiwa lakini, Ntinika na kamati yake ya ulinzi na usalama haikufika eneo hilo na badala yake aliamua kuwaita viongozi wa wafanyabiashara hao kwenda ofisini kwake kuzungumza upya suala hilo.

Alipoulizwa sababu za kushindwa kufika katika soko hilo kuzungumza na wafanyabiashara, Ntinika alisema kuna mambo yaliyomfanya kuahirisha ratiba ya kwenda kuonana na kuzungumza nao na badala yake alimtaka katibu tawala wilaya hiyo, Hassan Kawawa kuwapigia simu viongozi wa soko hilo ili wafike ofisini kwake.

Akizungumzia wito huo, Ngogo alisema baada ya kupigiwa simu na katibu huyo wa tawala, waliwapa taarifa wafanyabiashara lakini waliwazuia kwenda wakiutaka uongozi wa Serikali kwenda kuzungumza nao kama ulivyoahidi na si vinginevyo.

“Sisi viongozi tunasikiliza kauli ya wafanyabiashara na si vinginevyo, hivyo wametuzuia kwenda na sasa tunaendelea na shughuli nyingine na kila mfanyabiashara yupo eneo lake anaendelea na ujenzi,” alisema.

Mmoja wa wafanyabiashara hao ambaye aligoma kutaja jina lake alisema ni ngumu kusubiri tamko la Serikali la kukubaliwa au kukataliwa kujenga vibanda vyao vya kudumu kwani maisha yao yanatengemea biashara.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukiomba Serikali ituruhusu tujenge vibanda vya kudumu lakini imekuwa na kigugumizi kutupa jibu hadi majanga haya yanaendelea kujitokeza na sisi hapa tunakula leo kwa vile jana tuliuza. Sasa tangu Jumatano hatujauza halafu unatwambia tusubiri siku tano unafikiri tutakula wapi, lakini hayo majibu yatakuwa na fidia juu ya kuunguliwa kwetu?,” Alihoji mfanyabiashara huyo ambaye alikuwa katika harakati za ujenzi wa kibanda chake cha kudumu.