VIDEO: Soud Brown aachiwa kwa dhamana

Muktasari:

Mtangazaji wa Clouds katika kipindi cha Shilawadu, Soud Kadio ‘Soud Brown’ aliyekamatwa siku tano zilizopita na kuwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam, amefikishwa leo Septemba 24, 2018, mahakamani alikosomewa shtaka moja la kutumia maudhui mtandaoni bila ya kuwa na kibali.

Dar es Salaam. Mtangazaji wa Clouds kipindi cha Shilawadu, Soud Kadio ‘Soud Brown’ amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kutumia maudhui mtandaoni bila ya kuwa na kibali.

Hata hivyo mshitakiwa huyo alikamilisha masharti na kupewa dhamana.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nguka akishirikiana na Wakili Estazia Wilson walimsomea shtaka hilo Soud Brown leo Septemba 24, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustino Rwizile.

Nguka amedai kati ya Juni 11 na Septemba, 2018 Dar es Salaam kwa kutumia online Tv inayojulikana kwa jina la Shilawadu Tv,  kinyume cha sheria alitoa maudhui katika mtandao huo bila ya kuwa na kibali kutoka mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Baada ya kusomewa shtaka hilo mshtakiwa huyo alikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hata hivyo wakili Peter Kibala anayemtetea Soud Brown aliomba mteja wake huyo apewe dhamana kwa sababu shtaka linadhaminika.

Hakimu Rwizile akitoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa huyo alimtaka awe na mdhamini mmoja ambaye atasaini bondi ya Sh2 milioni, pia mshtakiwa mwenyewe  asaini bondi ya Sh2 milioni.

Soud Brown alifanikiwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana na kuachiwa huru na kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 18, 2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.