Sumaye, Lukuvi waongoza mazishi ya Mungai

Muktasari:

Mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana wa Chadema (Bavicha), Joseph Kasambala jana alijikuta katika wakati mgumu wakati alipotaka kuweka saini kwenye kitabu cha maombolezo ya Mungai kutokana na kuvalia magwanda ya chama hicho.

Mafinga. Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wameongoza mazishi ya mwanasiasa mkongwe nchini, Joseph Mungai

Mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana wa Chadema (Bavicha), Joseph Kasambala jana alijikuta katika wakati mgumu wakati alipotaka kuweka saini kwenye kitabu cha maombolezo ya Mungai kutokana na kuvalia magwanda ya chama hicho.

Mjumbe huyo alifika katika eneo hilo akiwa ameongozana na Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick Ole Sosopi, lakini askari walimzuia bila kueleza sababu.

Kasambala alizozana kwa muda na ofisa wa Polisi kabla ya askari huyo kumruhusu kutimiza azima yake. Msiba huo ulihudhuriwa na mamia ya waombolezaji wengi wao wakiwa ni wafuasi wa vyama vya CCM ambacho alikuwa kada wake mwandamizi na wa Chadema ambao walifika kwa wingi huku wakiwa wamevalia sare za chama chao. Licha ya kwamba waziri huyo wa zamani alikuwa mwanaCCM, katika kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana, alisimama katika jukwaa la Chadema kumnadi mtoto wake, William Mungai aliyekuwa akiwania ubunge wa Jimbo la Mafinga Mjini kupitia chama hicho kikuu cha upinzani.

Mungai alizikwa jana kwa heshima zote za Serikali.

Akizungumza kwenye msiba huo, Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chadema na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisema Mungai alikuwa kiongozi aliyependa kuwatumikia watu na alipenda kutenda haki. “Nimekuja hapa kwa sababu mbili; moja nilifanya kazi na Mungai nikiwa waziri mkuu na yeye akiwa waziri wa elimu katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Mungai alikuwa mmoja wa viongozi waliopenda kutenda haki, alikuwa akiona jambo anakuja kutoa ushauri hata kama lilikuwa na masilahi kwa chama cha upinzani,” alisema Sumaye.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Rajabu Luhwavi alisema Mungai amehusika kwa kiwango kikubwa kukijenga chama na Serikali na kwamba kwa wakazi wa Mufindi, Iringa na Taifa wanayo haki ya kujivunia.

Akitoa salamu za Serikali, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema Mungai ameacha pengo mkoani Iringa. Alisema hakuna mtu mwenye historia kubwa kama yake katika masuala ya siasa na utawala serikalini. Baadhi ya viongozi wengine waliohudhuria msiba wa Mungai ni Waziri wa Elimu, Joyce Ndalichako na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa.