Sura mpya kesi ya Babu Seya na mwanae

Wakili Donald Deya anayewatetea Nguza Viking na mwanae Johnson Nguza katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana. Na Mpiga Picha Wetu

Muktasari:

  • Hoja ambazo zimekubaliwa ni pamoja na mlalamikaji Nguza kutopimwa nguvu za kiume kama alivyokuwa ameomba, kutopata maelezo ya mashahidi na kutopata fursa ya kuwauliza maswali waliotoa ushahidi ili kuthibitisha makosa.

Arusha. Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu (AfCHPR), imekubali hoja tatu kati ya nane za ukiukwaji wa haki za binadamu katika hukumu ya kifungo cha maisha kwa mwanamuziki Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mtoto wake, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya ubakaji na ulawiti.

Hoja ambazo zimekubaliwa ni pamoja na mlalamikaji Nguza kutopimwa nguvu za kiume kama alivyokuwa ameomba, kutopata maelezo ya mashahidi na kutopata fursa ya kuwauliza maswali waliotoa ushahidi ili kuthibitisha makosa.

Mahakama hiyo ilitupa hoja tano za walalamikaji hao ambao jana hawakuwapo wakati uamuzi huo ukitolewa ambazo ni pamoja na kutolewa magereza ikisema haikuwa na mashiko tena, kutoridhishwa na mwenendo wa kesi katika Mahakama, kutopata fursa ya kujitetea wakati wa mwenendo wa kesi na kupata msaada wa kisheria; na kukosa haki ya kuwa na familia zao.

Akisoma hukumu katika kesi hiyo, iliyochukua dakika 55, Jaji Gerard Niyungeko kwa niaba ya majaji wenzake saba wa Mahakama hiyo, alisema kutokana na hoja hizo nane, zilizowasilishwa mahakamani hapo katika shauri hilo namba 006/2015, imejiridhisha kwamba tano hazikuwa na ukiukwaji wa haki hasa kutokana na maelezo ya walalamikaji.

Hoja zilizokubaliwa

Jaji Niyungeko, ambaye ni raia wa Burundi alisema jopo hilo la majaji limejiridhisha pasipo shaka kwamba hoja tatu zilizowasilishwa na walalamikaji zilikuwa na mashiko.

Hoja ambazo Mahakama hiyo imezikubali ni ile iliyowasilishwa na walalamikaji kwamba mtuhumiwa wa kwanza, Nguza wakati wa mwenendo wa kesi hiyo, alieleza kuwa hana nguvu za kiume na hivyo asingeweza kufanya vitendo vya ubakaji na alitaka mahakama kutoa agizo la kupimwa na madaktari hatua ambayo haikukubalika.

Jaji Niyungeko alisema hoja nyingine ambayo ilibainika kuwa na mashiko ni kuwa walalamikaji hawakupata maelezo ya mashahidi.

Jaji Niyungeko alisema wamekubaliana na hoja kuwa watuhumiwa ambao sasa wapo huru kutokana na msamaha wa Rais, hawakupata fursa ya kuwauliza maswali waliotoa ushahidi ili kuthibitisha makosa jambo, ambalo ni kosa.

Hoja zilizotupwa

Jaji Niyungeko alisema, baada ya uchambuzi wa hoja katika shauri hilo, wamebaini ombi la kwanza lilikuwa ni la kutolewa magereza ambalo hata hivyo, tayari watuhumiwa walitolewa kutokana na msamaha wa Rais John Magufuli.

Wanamuziki hao walipata msamaha huo Desemba 9, mwaka jana wakati Rais Magufuli alipowasamehe wafungwa 8,157 wakati akihutubia maadhimisho ya sherehe ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika mjini Dodoma.

Pia, Jaji Niyungeko alisema mahakama hiyo imejiridhisha kuwa mwenendo wa kesi katika shauri hilo kuanzia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahakama Kuu hadi Mahakama ya Rufaa ulikuwa wa haki tofauti na hoja za walalamikaji kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu hasa kutokana na ushahidi uliofikishwa mbele yake.

Alisema katika kuthibitisha kuwa mwenendo wa kesi hiyo ulikuwa wa haki, kulikuwa na tuhuma 21, lakini hadi hukumu ilipotolewa, zilikuwa zimebaki nne tu ambazo ndizo zilizowatia hatiani.

Alisema pia kitendo cha Mahakama za Tanzania, kuwaachia washtakiwa wengine watatu katika shauri hilo kinaonyesha kwamba mwenendo wa kesi ulikuwa wa haki na hakukuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Jaji Niyungeko alisema Mahakama hiyo pia imetupa hoja kuwa watuma maombi hawakupata fursa nzuri za kujitetea wakati wa mwenendo wa kesi hiyo.

Jaji Niyungeko, alisema hoja kuwa Nguza na Johnson hawakupata msaada wa kisheria, imetupwa kwa kuwa kulikuwa na uwakilishi wa kisheria.

Alisema pia hoja ya kuwa uamuzi wa kesi hiyo, ulikiuka mkataba wa kuanzishwa mahakama hiyo haikuwa sahihi kutokana na kukosekana ushahidi uliofikishwa mahakamani hapo.

Kadhalika, alisema hoja kwamba wakati wa mwenendo wa kesi hiyo walalamikaji walikosa haki yao ya kikatiba ya kuwa na familia zao na kuendelea na shughuli zao pia imeonekana kukosa ushahidi wa athari hizo kutokana na maelezo yaliyofikishwa mahakamani.

Fidia ya gharama za kesi

Akizungumzia hoja ya kulipwa fidia kutokana na gharama za kesi hiyo na madai mengine, Jaji Niyungeko alisema Mahakama imetoa mwezi mmoja kwa walalamikaji, kuwasilisha mahakamani hapo madai yao ya fidia kama watahitaji na kutoa muda kama huo kwa Serikali kuyajibu kabla ya kutoa uamuzi juu ya madai hayo ya fidia.

Katika kesi hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alikuwa anawakilishwa na mawakili, Sara Mwaipopo, Nkasori Sarakikya, Baraka Luguna, Elisha Suka na Aida Kisumo.

Upande wa walalamikaji uliwakilishwa na mwanasheria na ofisa mtendaji mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Afrika (Palu), Donald Deya.

Akizungumza baada ya uamuzi huo, Deya alisema ameridhishwa na anasubiri nakala ya hukumu ili kuteleza maagizo ya mahakama baada ya kushauriana na wateja wake.

“Siwezi kusema lolote kwa sasa, juu ya msimamo wa wateja wangu kwani hawajanipa mamlaka hayo,” alisema.

Ilivyokuwa

Babu Seya na wanae watatu walikamatwa Oktoba 12, 2003 na kufikishwa kituo cha Polisi cha Magomeni jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na tuhuma za ubakaji na ulawiti wa watoto wa kike wenye umri wa chini ya miaka 10.

Oktoba 16, 2003 wapandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa jumla ya mashtaka 21, kati ya hayo 10 ya ubakaji wa watoto hao na mengine 11 ya kuwanajisi

Baada ya kuwa wamesota mahabusu wakati kesi yao ikiendelea kusikilizwa, Juni 25, 2004 Mahakama ya Kisutu iliwahukumu adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Kwa nyakati tofauti walikataa rufani Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa na kugonga mwamba.