TBA: Serikali inalipia majengo ya Udom inayoyatumia

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Majengo Tanzania  (TBA), Elius Mwakalinga amesema Serikali inalipia majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambayo yanatumika kama ofisi za wizara.

Muktasari:

  • Akizungumza ofisini kwake juzi, Mwakalinga alisema TBA ina mipango ya kuboresha na kujenga majengo mengine, lengo likiwa ni kila wizara kuwa na yake.
  • Alisema anaamini hatua hiyo ya Serikali inapunguza ukali wa deni la mkopo uliotumika kugharamia ujenzi na kwamba ni ya muda.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Majengo Tanzania  (TBA), Elius Mwakalinga amesema Serikali inalipia majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambayo yanatumika kama ofisi za wizara.

Akizungumza ofisini kwake juzi, Mwakalinga alisema TBA ina mipango ya kuboresha na kujenga majengo mengine, lengo likiwa ni kila wizara kuwa na yake.

Alisema anaamini hatua hiyo ya Serikali inapunguza ukali wa deni la mkopo uliotumika kugharamia ujenzi na kwamba ni ya muda. 

“Hatua hii imesaidia kwa sababu  kwa watu binafsi wangetaka malipo ya pango kwa mkupuo. Huku watalipia kidogokidogo nasi tunashughulikia jambo hilo kwa namna nyingine ikiwamo kuchukua jengo la Posta ya Zamani Dodoma tumepata fedha za kulikarabati,” alisema.

Mwakalinga alisema jengo hilo lina ghorofa nne na Sh35 bilioni zimetengwa kwa kazi hiyo, hivyo wanatarajia likikamilika litasaidia katika utekelezaji wa mpango wa awamu ya pili wa Serikali kuhamia Dodoma. Alisema ukarabati utakamilika Juni.