TCRA yataja changamoto tano uendeshaji kesi makosa ya mtandao

Muktasari:

Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki katika warsha ya kukuza uelewa wa matumizi sahihi ya mitandao iliyoandaliwa na kampuni ya Kingdom Heritage inayojishughulisha na utoaji wa elimu kuhusu masuala hayo.

 Wakati Serikali ikielekeza nguvu kukabiliana na makosa ya mtandao, Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetaja changamoto tano za uendeshaji kesi zinapofikishwa mahakamani.

Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki katika warsha ya kukuza uelewa wa matumizi sahihi ya mitandao iliyoandaliwa na kampuni ya Kingdom Heritage inayojishughulisha na utoaji wa elimu kuhusu masuala hayo.

Changamoto hizo zimetajwa kuwa ni uelewa mdogo wa majaji, mahakimu na wanasheria; ushahidi wa kuwasilishwa; kufutika kirahisi; uchunguzi; na wapi pa kupeleka malalamiko.

Mwanasheria mwandamizi kutoka TCRA, Dk Philip Philikunjombe alisema kabla ya majaji, mahakimu na wanasheria kupewa dhamana ya kusikiliza kesi hizo, ni lazima wajengewe uelewa juu ya namna ya kuziendesha.

“Hapa kuna wakati mambo huwa magumu, unaweza kukuta kesi inaendeshwa mpaka unajiuliza hivi ni kweli haya ndiyo yanayotakiwa kufanyika? Kama hatutawajengea uelewa watu hawa itakuwa vigumu kushughulikia kesi hizi na kutakuwa na makosa makubwa yanayotendeka,” alisema Dk Philikunjombe.

Mbali ya hilo, alisema bado kuna ugumu wa kujua ni namna gani ushahidi unatakiwa kuwasilishwa mahakamani pindi mtu atakapokwenda kulalamika kuwa katendewa makosa. “Umetukanwa kwenye simu je, upeleke simu ya aliyekutukana mahakamani! Tutajuaje kama baada ya kumnyang’anya simu yake hukubadilisha ujumbe. Kama umechapisha katika karatasi, tutajuaje kama hukuongeza maneno au kupunguza? Hivyo, bado ni vigumu kupata ushahidi wa kesi hizi,” alisema.

Changamoto nyingine alisema ni ushahidi wa kesi hizo kuharibika kirahisi kwa sababu mtuhumiwa anaweza kufuta ujumbe hivyo haitakuwa rahisi kuthibitisha makosa hata kama ujumbe huo atakuwa nao mlalamikaji.

“Labda kama tungekuwa na vitengo maalumu vya wataalamu wa teknolojia wa kuweza kufanya uchunguzi kwa kina ili kubaini ni kweli ujumbe ulikuwapo na ukafutwa au kubadilishwa,” alisema Dk Philikunjombe.

Nyingine alisema ni uchunguzi wa makosa hayo yanapotokea.

“Kila siku teknolojia inabadilika, ni lazima kuendana na mabadiliko hayo kwa kuwa na vifaa vyenye teknolojia ya hali ya juu ambavyo vitakuwa na uwezo wa kuthibitisha makosa hata kama ujumbe umefutwa au kubadilishwa,” alisema Dk Philikunjombe.

Alisema waathirika wa makosa ya mtandao bado wanapata wakati mgumu kutokana na kutojua ni wapi wanapaswa kupeleka malalamiko yao. “Sheria inasema ukitendewa kosa katoe taarifa kituo cha polisi kilicho karibu yako. Sasa umetukanwa mtandaoni wewe upo Dar es Salaam, aliyekutukana yupo Arusha, aliyesaidia kufikisha ujumbe yupo Kigoma kesi itatatuliwa katika mahakama gani?” alihoji.

Alisema nchi bado ina safari ndefu kuhakikisha inakabiliana na makosa ya mtandao ambayo yamekuwapo tangu zamani.

“Inahitajika elimu ya kutosha juu ya jambo hili kwa sababu zaidi ya asilimia 95 ya makosa hayo yalikuwapo tangu zamani, ni machache tu ndiyo mapya,” alisema Dk Philikunjombe.

Akizungumzia uzoefu wake juu ya usikilizwaji wa kesi za makosa ya mtandao, mwanzilishi wa mtandao wa JamiiForums, Mexcence Melo alisema ipo haja ya wasimamizi wa kesi kupatiwa elimu ya sheria zinazohusu makosa ya mtandao ili haki iweze kutendeka.