Friday, July 21, 2017

TGGA yajitosa katika mbio za kumkomboa mtoto wa kike nchini

 

Mlezi Mstaafu wa Chama cha Maskauti wa Kike

  Mlezi Mstaafu wa Chama cha Maskauti wa Kike Tanzania, Mama Salma Kikwete, akimvisha skafu mlezi mpya wa chama hicho, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan katika hafla kumsimika rasmi iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Picha na Emmanuel Herman 

By Kelvin Matandiko,Mwananchi kmatandiko@mwananchi.co.tz

Mtoto wa kike wa Kitanzania ni yupi, yuko wapi na ana ulinzi gani? Nani anawajibika na kwa nini kuna umuhimu wa kufanya hivyo katika uhusiano wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi?

Ni baadhi ya maswali yanayohitaji majibu kutoka kwa kila Mtanzania bila kujali mwenye uzazi au asiyekuwa na uzazi.

Hali ya usalama kwa mtoto wa kike hapa nchini imeendelea kutoridhisha wengi kutokana na kuibuka kwa matukio mbalimbali ikiwamo ndoa za utotoni, mimba za utotoni, ukeketaji, vikwazo vya elimu pamoja na ubakaji.

Matoleo mbalimbali ya utafiti yanaonyesha kwamba jamii inaendelea kuongeza uelewa dhidi ya matukio hayo licha ya baadhi ya watu katika jamii hizo hizo kuendelea na ukatili huo.

Taasisi, asasi za kiraia, vyama, mashirika na wanaharakati mbalimbali wanawake wameendeleza kampeni mbalimbali ikiwamo ya mtoto wa mwenzio ni wako, ukisomesha mtoto wa kike umeelimisha taifa, sidanganyiki na piga vita ukatili wa kijinsia.

Jumatano iliyopita, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na mke wa Rais wa Awamu ya Nne, Salma Kikwete walikutana uso kwa uso na kutangaza vita ya kuendeleza mapambano hayo kupitia Chama cha Maskauti wa Kike Tanzania (TGGA).

Katika tukio hilo, Salma Kikwete alikuwa akikabidhi kijiti cha Mlezi wa TGGA kwa Samia Suluhu baada ya kuwa mlezi wa chama hicho kwa miaka 12. 

Chama hicho kilichoanzishwa hapa nchini mwaka 1928, majukumu yake yamekuwa ni kutoa elimu ya ujana na kujikinga na ugonjwa wa HIV/AIDs, matumizi ya dawa za kulevya na pombe, kuzuia mimba za utotoni na afya bora, elimu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na kujiamini.

Katika tukio hilo, Mama Salma anaeleza changamoto zinazomtesa mtoto wa kike kwa sasa ni pamoja na matumizi ya mitandao, yanayotokana na ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano. Pia, kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo.

Mama Salma ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa, kwa sasa anatoa wito kwa Watanzania kila mmoja kuhusika katika ulinzi wa mtoto wa kike huku akitahadharsha watoto hao wa kike kuwa makini katika matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii. Anawataka kuchuja maarifa mazuri na kuacha yasiyofaa.

 “Lakini pia mnatakiwa (watoto wa kike) kujihadhari na magonjwa ikiwamo gonjwa la Ukimwi, ugonjwa huu upo na ni ugonjwa hatari sana,” anasema kwa msisitizo akiwaeleza wanafunzi wa kike waliokuwa wakimsikiliza. 

Kwa upande wake, Samia Suluhu anasema bila Mama Anna Abdalah asingeweza kufikia mafanikio aliyonayo katika uongozi na kutambuliwa kama makamu wa rais kwa sasa. Anasema malezi aliyoyapata kutoka kwa walezi ndani ya TGGA ni msingi unaoweza kumjenga mtoto wa kike katika maisha yake.

“Kuna msemo unasema ‘Dunia hadaa ulimwengu shujaa’, naomba msihadaike na vishawishi vya dunia, ni vyema kuwa makini sana na kujihadhari juu ya vishawishi, TGGA ni jukumu lenu kuwalea vijana wetu katika malezi na maadili mema, ni tegemeo la kesho,” anatoa ujumbe wake kwa mtoto wa kike.

Anasema hakuna Serikali inayoweza kujivunia katika kumaliza changamoto za mtoto wa kike lakini kila inayoingia imekuwa ikitekeleza kwa nafasi yake katika vita hiyo. “Tanzania tumepiga hatua kubwa ukilinganisha na mataifa mengine lakini bado tutaendelea kuweka mazingira na ulinzi wa kumsaidia mtoto wa kike,” anasema.

Ukombozi wa mtoto wa kike

Shirika la Afya Duniani (WHO) katika utafiti uliochapishwa Januari, 2016 liliitaja Tanzania kuwa  kati ya nchi tatu barani Afrika kwa ndoa na mimba za utotoni kwa asilimia 28.

Pia, Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), linabainisha katika taarifa zake kuwa kwa wastani watoto wa kike wawili kati ya watano huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Takwimu za utafiti wa Idadi ya Watu na Afya Tanzania (TDHS, 2010) zilibaini kuwa asilimia 37 ya watoto wa kike Tanzania huolewa kabla ya kufikisha miaka 18.

Shirika la Watoto Duniani (UNICEF 2012) liliainisha mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni kuwa ni Shinyanga (59), Tabora (58), Mara (55), Dodoma (51), Lindi (48) na Morogoro (42).

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alinukuliwa na gazeti hili miezi kadhaa iliyopita akisema Serikali ina mpango wa kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 27 ya mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 13.

Pia, itapunguza ukatili asilimia 39 mpaka asilimia 20 na kupunguza ukatili wa kingono kwa watoto wa kike kutoka asilimia 33 hadi kufikia asilimia 16 na kwa watoto wa kiume kutoka asilimia 14 hadi asilimia saba.

Kwa upande wake Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama) anasema familia na jamii kwa ujumla wana jukumu la kumlinda mtoto wa kike. “Katika chama, kasi ya usajili wa wanachama ambao ni wanafunzi inaongezeka na wanachama wapya 2797 wataapishwa mkoa wa Lindi siku chache zijazo, tunataka idadi iongezeke zaidi ili mtoto wa kike anufaike.”

Mama Salma anasema idadi ya wanachama wake imeendelea kuongezeka kutoka 97,143(2015) hadi kufikia 100,080 kwa mwaka huu huku wapya 300 wakitarajia kuapishwa. Asilimia 95 ya wanachama wake ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari huku asilimia tano wakitoka nje ya mfumo huo.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sofia Mjema anapendekeza kila mkuu wa wilaya awe mlezi wa TGGA katika eneo lake na awajibike kupanua mtandao huo wa TGGA ili kuwasaidia watoto wa kike kupitia chama hicho.

Mwanasiasa mkongwe na Kada wa CCM,  Anna Abdallah anasema miongoni mwa vikwazo katika chama hicho ni kuendelea kuwapo kwa mfumo dume katika jamii.

“Jamii kwa sehemu kubwa bado inasumbuliwa na mfumo dume, kwa hiyo juhudi bado zinahitajika, jamii ielimishwe zaidi ili kukomesha mfumo huo,” anasema.

Mbinu za kujiendesha TGGA

Samia anatoa maagizo matatu kwa uongozi wa TGGA kubuni mbinu zitakazosaidia kujitegemea badala ya kutegemea wahisani pekee.

Mbinu hizo ni kutumia ardhi iliyopo kwa kukopa au kuingia ubia na kampuni zilizotayari kushirikiana ili kuanzisha miradi ya majengo ya kibiashara.

Pili, kuongeza usajili wa wanachama wapya, watakaosaidia kuongeza mapato yatokanayo na ada za kujiunga na mwisho ni kuanzisha utaratibu wa kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa wanafunzi wanaoishia darasa la saba na kidato cha nne.

 “Mafunzo kama kushona vitambaa na kutengeneza bidhaa ambazo zitauzwa, yatasaidia mabinti kuendeleza maisha yao, kuongeza kipato na kujiepusha na vishawishi vya kuingia kwenye mapenzi katika umri mdogo, itapunguza mimba za utotoni na uvunjifu wa amani,”anasema Samia.

Ukipata mimba hakuna kuendelea na shule

Katika hatua nyingine, Anna Abdallah ambaye ni mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa TGGA, anasisitiza zuio la mtoto wa kike kutoendelea na masomo endapo atapata ujauzito.

Anna anaunga mkono kauli ya Rais John Magufuli akisema badala ya kuendelea kuishambulia Serikali, jamii inatakiwa imsaidie mtoto wa kike asipate ujauzito wakati wa masomo yake.

Rais Mgufuli kwa nyakati tofauti alinukuliwa akitoa tamko kwamba katika uongozi wake, hakuna mwanafunzi wa kike atakayerudi kuendelea na masomo baada ya kupata ujauzito, kauli ambayo ilionekana kupingwa na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu na watetezi wa haki za binadamu.

“TGGA inaungana na tamko hilo na Rais ametoa tamko hilo wakati muafaka ili wadau wote sasa tujipange kuongeza uelimishaji zaidi, na hii ni kazi mojawapo ya TGGA, kwa hiyo tusipige kelele tu,” anasema.

-->