TTB: Kupatwa kwa jua kutainua utalii kusini

Kaimu mkurugenzi mwendeshaji wa TTB, Philip Chitaunga  (katikati) akizungumza na wanahabari leo

Muktasari:

Jua litapatwa Septemba Mosi, mwaka huu ambapo maeneo ya Wanging’ombe huko Njombe na Rujewa mkoani Mbeya na maeneo yasiyozidi kilomita 100 yashuhudia giza kwa dakika kadhaa huku maeneo mengine ya nchi yakishuhudia kufifia kwa jua.

Bodi ya Utalii nchini (TTB) imesema tukio la kupatwa kwa juai litafungua milango kwa sekta ya utalii katika Nyanda za Juu Kusini kwa kuwa watalii na watafiti kutoka ndani na nje ya nchi watembelea maeneo hayo kushuhudia tukio hilo la kipekee duniani.

Jua litapatwa Septemba Mosi, mwaka huu ambapo maeneo ya Wanging’ombe huko Njombe na Rujewa mkoani Mbeya na maeneo yasiyozidi kilomita 100 yashuhudia giza kwa dakika kadhaa huku maeneo mengine ya nchi yakishuhudia kufifia kwa jua.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo, kaimu mkurugenzi mwendeshaji wa TTB, Philip Chitaunga amesema TTB imeandaa safari ya watu 50 itakayowajumuisha wanahabari na watu maarufu nchini kwenda kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

“Sekta ya utalii ndiyo inayoongoza kuiingizia nchi pato la kigeni…hivyo tukio hili tunaliona kama ni fursa itakayoutangaza utalii wa kusini. Kusini kwa sasa miundombinu ni mizuri, kuna uwanja mkubwa wa ndege, barabara zinapitika hivyoTanzania itafahamika zaidi,” amesema Chitaunga.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano juu ya tukio hilo, mtaalamu wa Idara ya Sayansi na Mazingira ya Chuo Kikuu Huria (OUT) Dar es Salaam, Dk Noorali Jiwaji amesema tukio litaanza kuonekana saa 4:17 asubuhi hadi saa 7:55 mchana.

Kwa mujibu wa mtaalam huyo, japokuwa maeneomengi ya nchi yatashuhudia utofauti mfano jua kufifia, lakini maeneo ya kusini mwa nchi hususani Mbeya na mikoa ya jirani ikiwemo Katavi, Rukwa, Mbeya, Njombe, Ruvuma na Mtwara itashuhudia giza kwa takribani saa nne.

Wataalam wa OUT wakiongozwa na Dk Jiwaji wamechagua mji wa Rujewa, uliopo wilaya ya Mbarali, mkoa wa Mbeya kuwa sehemu ya kuratibu tukio hilo la kihistoria.

Sababu za kuchagua eneo hilo ni kwamba hakuna wasiwasi wa kuathiriwa na hali ya hewa kama vile uwepo wa mawingu. “Uwezekano wa mawingu katika eneo hilo ni asilimia 20 tu hivyo hakuna wasiwasi kuwa tutashindwa kushuhudia tukio hilo,” Dk Jiwaji anafafanua.

Watu watakaokuwa maeno hayo na maeneo ya karibu siku hiyo, umbali usiozidi kilomita 100 wakitazama angani kwa kutumia miwani maalum, wataona mwezi umelifunika jua na kuacha umbo la pete. Inamaanisha kuwa tofauti mwaka 1980 ambapo jua lilipatwa “kikamilifu”, Septemba Mosi, mwaka huu halitafunikwa lote.