TWB kunadi mali za wadaiwa sugu


Muktasari:

Wadaiwa hao wapatao 7000 watajikuta katika wakati mgumu kwa kuwa na mikopo inayotajwa kuwa ni chechefu.

Dar es Salaam. Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) imetangaza kuzipiga mnada mali za wadaiwa sugu 7,065 watakaoshindwa kulipa madeni yao ndani ya siku saba kuanzia leo.

Mwenyekiti wa bodi wa benki hiyo, Beng’i Issa amesema leo Machi 6 kwamba  uamuzi huo ni sehemu ya kukabiliana na ongezeko la mikopo chechefu au isiyolipika iliayo.

“Mpaka sasa mikopo isiyolipika imefia Sh7.9 bilioni hivyo kuongeza ugumu kidogo katika kuhakikisha tunapata mtaji wa kutosha,” amesema Issa.

Ndani ya muda walioutoa, alisema wateja wanaodaiwa wanapaswa kulipa madeni yao ambayo ni ya muda mrefu.

“Wengi wameshapitiliza siku 90 za kutorejesha madeni yao kinyume na utaratibu na makubaliano na benki,” amesema

Kwa watakaoshindwa kulipa fedha hizo ndani ya muda uliotolewa wa benki kuchukua hatua za kisheria kabla ya kunadisha dhamana zao, amesema wenye dhamira ya kulipa waende kwenye tawi lolote la benki hiyo wakiwa na mpango mahususi wa jinsi watakavyofanikisha malipo yao.

Januari 4, wakati Benki Kuu Tanzania (BoT) inatangaza kufuta leseni za baadhi ya benki nchini, TWB ilipewa agizo la kuongeza mtaji ndani ya miezi sita ili kukidhi mahitaji ya ukwasi unaohitajika.

Kulingana na masharti ya taasisi za fedha na benki za biashara nchini, kila moja inatakiwa kuwa na mtaji na ukwasi wa kutosha kukidhi mahitaji ya kila siku.

Wakati TWB ikipewa onyo hilo, benki za Covenant, Efatha, Benki ya Wananchi Njombe, Kagera Farmer’s Cooperative Bank na Benki ya Wananchi Meru zilifutiwa leseni.

Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania, Japhet Justine amesema  sheria inawaruhusu kuuza mali au dhamana za wateja walizoweka endapo watashindwa kurejesha mkopo kwa wakati waliokubaliana.

“Mbali na kupiga mnada mali zao, taarifa zao tutazipeleka Benki Kuu ya Tanzania wasiweze kupata mkopo katika benki nyingine yoyote nchini,” amesema Justine.

Amesema tangu kutolewa kwa taarifa ya awali kuwa benki ipo katika hali mbaya, wamekusanya zaidi ya Sh2 bilioni kutoka kwa wadaiwa walionao, hatua ambayo alisema ni nzuri.

Kwa sasa, alisema wapo katika maongezi na wadau mbalimbali kuwawezesha kupata mtaji waliowekewa na Benki Kuu na kwamba mwelekeo unaonekana kuwa mzuri.

“Baada ya benki yetu kupewa maagizo ya kuongeza mtaji na Benki Kuu tunapokea wateja na wageni wengi wanaohitaji ufafanuzi kuhusu fedha zao lakini wote wanaelewa,” ameongeza.