Tuesday, January 9, 2018

Taasisi nne zajitosa kudhibiti ujangili

Mkurugenzi mtendaji wa Chemchem Foundation

Mkurugenzi mtendaji wa Chemchem Foundation Riccardo Tosi akimkabidhi  msaada wa vitabu 500  kwa ajili ya shule ya msingi Tarangire na Kakoi kwa Mwenyekiti wa kikundi cha wanawake Kakoi Veronica Loshiye. Picha Mussa Jum 

By Mussa Juma, Mwananchi mjuma@mwananchi.co.tz

Babati. Mfuko wa Kusaidia Uhifadhi katika kampuni ya Chemchem ambayo imewekeza eneo la Hifadhi ya Jamii Burunge wilayani Babati umepanga kutumia zaidi ya Sh165 milioni mwaka 2018 katika vita dhidi ya ujangili.

Mkurugenzi mtendaji ya Chemchem Foundation, Riccardo Tosi alisema wameamua kuongeza fedha ili kumaliza tatizo la ujangili hasa wa vitoweo katika eneo hilo.

Alisema kwa miaka mitatu iliyopita wamekuwa wakitumia kila mwaka wastani wa Dola 30,000 za Marekani (zaidi ya Sh65 milioni) katika vita dhidi ya ujangili lakini mwaka huu watatumia Dola 82,000 (zaidi ya Sh165 milioni).

Tosi alisema mfuko huo kwa kushirikiana na askari wa Burunge WMA, Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujangili (KDU) Kanda ya Kaskazini na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) wamejipanga kuimarisha ulinzi katika eneo hilo.

“Tutaimarisha ulinzi, doria na matumizi ya vifaa vya kisasa katika kupambana na ujangili na kuimarisha uhifadhi katika eneo hili ambalo ni mapito ya wanyama kutoka Tarangire kwenda Manyara,” alisema. Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Chemchem, Nicolaus Negri alisema katika eneo hilo changamoto kubwa ni ongezeko la mifugo ndani ya hifadhi na makazi kinyume cha taratibu.

“Sisi kama wawekezaji tunaongeza fedha za kupambana na ujangili lakini kama bado kuna uvamizi, mifugo na makazi kazi inakuwa ngumu kudhibiti majangili,” alisema.

Spika wa Burunge WMA, Ramadhani Ismail alisema kuwa mwaka 2018 wamejipanga kupambana na ujangili wa wanyama wadogo.

Alisema baada ya kufanikiwa kukomesha ujangili wa wanyama wakubwa kama tembo, nyati na twiga, ujangili ambao upo kwa sasa katika eneo hilo ni wa kutafuta nyama kwa ajili ya kitoweo.

“Tumenunua gari jipya za kufanya doria lakini pia tumekuwa na ulinzi wa pamoja baina yetu WMA, mwekezaji Chemchem na EBN, askari wa KDU na wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire,” alisema.

Burunge WMA ni miongoni mwa maeneo ya hifadhi ambayo yamekuwa yakisimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (Tawa).

-->