Taasisi tano zapata Sh12 bil za kutatua kero za mtoto wa kike

Mkuu wa Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF), David McGinty

Muktasari:

  • Hayo yalibainika jana katika Wiki ya Ubunifu iliyozinduliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

Dar es Salaam. Taasisi tano nchini zimepewa Sh12 bilioni kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazomkabili mtoto wa kike wakati wa ukuaji, mfumo wa majitaka na mazingira salama ya hedhi kwa mtoto wa kike.

Hayo yalibainika jana katika Wiki ya Ubunifu iliyozinduliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

Akizungumza katika uzinduzi huo, kiongozi mkuu wa Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF), David McGinty alisema: “Tumewekeza ubunifu katika maeneo hayo ili kuwa na matokeo chanya kwenye maisha ya Watanzania, maeneo hayo yataleta majibu ya kukabiliana na changamoto za ukuaji wa mtoto, usalama wa hedhi kwa mtoto na usafi wa mazingira, itakayosaidia ustawi wa jamii,” alisema McGinty.

Taasisi tano zilizopata ufadhili awamu ya tatu ya uzinduzi huo ni Ubongo Learning, Hakielimu, Karibu Tanzania Organisation, Catholic Relief Services, D-Tree International na Dorcas Aid international Tanzania.

Akizungumzia uzinduzi huo, kaimu mtendaji mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu alisema ubunifu unahitaji mambo matatu ambayo ni mfumo, miundombinu na uwezeshaji wa rasilimali fedha.

Dk Nungu alisema ubunifu nchini ni chachu ya maendeleo katika sekta zote zinazogusa maendeleo ya jamii na kiuchumi.

“Teknolojia na ubunifu ni maeneo yenye mchango mkubwa katika kuimarisha ustawi wa maisha, kuimarisha na kuchochea ukuaji uchumi, kumaliza umaskini,” alisema Jane Miller, naibu mkuu wa Idara ya Kimataifa ya Maendeleo ya Uingereza (DFID).

Meneja wa utafiti na uchambuzi wa Shirika la HakiElimu, Godfrey Bonaventure alisema ubunifu wa mradi wa “Mwanzo bora” umesaidia kufikia shule 20 na walimu 80 wilaya za Iramba, Kilosa na Kinondoni.