Taasisi yasisitiza neema ya mikopo elimu ya juu

Muktasari:

  • Zaidi ya wanafunzi 50,000 hawatanufaika na mikopo hiyo kwa ajili ya kufanikisha kusoma katika vyuo vya elimu ya juu kwa mwaka 2017/18.

Dar es Salaam. Taasisi ya Msaada wa Kijamii Tanzania (TSSF) imesitaka wanafunzi waliokosa mikopo ya elimu ya juu kujitokeza kuomba ufadhili wanaoutoa kwa riba nafuu.

Zaidi ya wanafunzi 50,000 hawatanufaika na mikopo hiyo kwa ajili ya kufanikisha kusoma katika vyuo vya elimu ya juu kwa mwaka 2017/18.

Lakini taarifa iliyotolewa jana na mkurugenzi mkuu wa TSSF, Donati Salla inasema wanufaika ni wanafunzi wanaoendelea na masomo ngazi ya shahada na stashahada kutoka chuo chochote kinachotambulika na Serikali.

Pia, amesema mwanafunzi ambaye ana matarajio ya kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza mwaka wa masomo 2017/18 naye anaruhusiwa kutuma maombi ya mkopo huo.

Taarifa hiyo inasema mwombaji lazima awe na mdhamini ambaye ni mtumishi wa umma mwenye sifa ya umri wa kudumu kazini kwa kipindi kisichopungua miaka mitano kabla ya kustaafu.

“Umri huo unahesabiwa baada ya mwanafunzi kumaliza miaka miwili tangu alipohitimu masomo yake. Kama mwombaji ni mtumishi wa umma anaweza kujidhamini mwenyewe,” alisema Salla.

“Mwombaji ni lazima awe ni mwanafunzi anayeendelea au anayetarajia kujiunga na taasisi ya elimu ya juu ambayo ipo ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na mkopo huu ni maalumu kwa wanafunzi ambao hawana mkopo kabisa,” alifafanua.

Alisema mwombaji asiye na mdhamini mwenye sifa hizo, atapaswa kulipa ada ya dhamana ya mkopo atakayopewa na TSSF ambayo ni asilimia mbili ya mkopo kwa mwombaji ambaye atapata mkopo chini ya Sh4 milioni au asilimia 3 ya mkopo utakaoanzia Sh4 milioni.

Mkurugenzi mkuu huyo alifafanua aina za mikopo akisema TSSF inalipa gharama zote za mafunzo ya elimu ya juu kuanzia mwaka wa kwanza mpaka wa mwisho ambazo ni ada, chakula, malazi, vitabu, stesheni, posho ya mazoezi kwa vitendo na posho ya utafiti.

Alisema kipaumbele kitatolewa kwa wanafunzi waliokosa mikopo inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) na baada ya kuwahudumia hao watawafikiria waliopata mikopo kidogo kutoka HESLB.

Alisema kutakuwa na mkopo wa nyongeza ambao unagharimia sehemu ya mahitaji ya mwanafunzi anapokuwa chuoni kuanzia anapoomba mkopo huo hadi anapohitimu masomo.

“Mkopo huu ni maalumu kwa wanafunzi ambao wanafadhiliwa na HESLB kwa asilimia sifuri hadi 50 au analipiwa ada tu bila gharama za chakula na malazi au kulipiwa chakula na malazi bila ada,” alisema na kuongeza:

“Mkopo huu unahusu wanafunzi ambao wanatoka familia zenye kipato cha kati ambao wanaweza kujilipia sehemu ya gharama za masomo ila si zote. Mwombaji wa mkopo huu anapaswa kuomba hitaji lake moja kwa moja.”

Salla alisema waombaji wanaweza kutembelea tovuti ya TSSF na kwamba Novemba 30 kutakuwa na mkutano kati ya taasisi hiyo na wakuu wa taasisi za elimu ya juu utakaojadili masuala mbalimbali, hasa ushiriki wao katika utoaji mikopo.