Takukuru yatangaza kutoa Sh 10 milioni kwa atakayefanikisha kukamatwa mfanya kazi wake

Muktasari:

Naibu Mkurugenzi wa Takukuru, Brigedia Jenerali, John Mbungo amesema mfanyakazi huyo anatuhumiwa kujipatia mali nyingi  kinyume cha Sheria ya  Utumishi wa Umma.

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetangaza donge nono la Sh10 milioni kwa yoyote atakayefanikisha kukamatwa kwa aliyekuwa mfanyakazi wake Godfrey Gugai.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Novemba 14, Naibu Mkurugenzi wa Takukuru, Brigedia Jenerali, John Mbungo amesema Gugai anatuhumiwa kujipatia mali nyingi  kinyume cha Sheria ya  Utumishi wa Umma.

Amesema kwa nafasi ya Gugai ya  mhasibu wa taasisi hiyo ni vigumu kupata mali nyingi kiasi hicho.

"Awali tulipomhoji alitoa ushirikiano lakini tukiwa tunaendelea alitoweka na kwa taarifa tu amekuwa akitoka kwa magendo nje ya nchi, kwa yeyote atakayefanikisha kumpata tutamzawadia Sh10 milioni," amesema  Mbungo

Amesema baada ya kutoweka walikwenda mahakamani kuhusu mali zake na tayari kuna zuio la kutokufanya kitu chochote yaani visiuzwe au kuendelezwa.

Amezitaja baadhi ya mali anazomiliki mikoa mbalimbali ni nyumba zaidi ya  tano, viwanja zaidi ya 30 na magari matano.

"Kama atakuja na kutupa ushirikiano ikiwamo kuthibitisha uhalali wale basi tutamwachia mali yake lakini kwa nafasi yake kumiliki mali zote hizi zinatutia walakini," amesema

Naibu mkurugenzi huyo amewaonya watumishi wa umma kutokutumia vibaya madaraka yao waliyopewa kwani wakibainika hawatasita kuwachukulia hatua.