Takukuru sasa yatoa somo uchaguzi CCM

Muktasari:

  • Wakipewa elimu hiyo katika semina, waombaji hao wametakiwa kuepuka vitendo vya rushwa kipindi cha uchaguzi unaotarajia kuanza hivi karibuni.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewataka wanaoomba uongozi ndani ya CCM Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza kuacha kutoa hongo ili wachaguliwe.

Wakipewa elimu hiyo katika semina, waombaji hao wametakiwa kuepuka vitendo vya rushwa kipindi cha uchaguzi unaotarajia kuanza hivi karibuni.

Ofisa Mchunguzi wa Takukuru wilaya hiyo, Doreen Ntongazi alisema nia ya Serikali ni kuwapata viongozi watakaokemea vitendo vya rushwa badala ya kuviendekeza.

“Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007, kinatamka kuwa ni kosa kuchukua zawadi, manufaa au kitu chochote kinachohusiana na majukumu ya kikazi,” alisema Ntongazi.

Alifafanua kuwa kifungu hicho kinahusu makosa madogo madogo yanayotajwa kwa majina mbalimbali kama vile kitu kidogo na chai.

“Tukijiepusha na vitendo vya rushwa tutapata viongozi bora watiifu na wanyenyekevu... kipindi cha kampeni mnatoa ahadi nyingi baada ya kupata mnasahau kuzitimiza na kusababisha migogoro, ni kosa kutoa rushwa na kupokea,” alisema.

Katibu wa CCM Wilaya, Maulid Acheni alisema kwamba ni mwiko kwa kiongozi, mgombea au mwanachama kutoa na kupokea rushwa.

Alisema si tu wakati wa uchaguzi bali katika kipindi chote cha utumishi wao.