Takukuru waendelea kuhangaika na jalada la Mnyeti

Muktasari:

Mnyeti ambaye kabla ya kutuhumiwa kutoa rushwa alikuwa ni mkuu wa wilaya ya Arumeru, anadaiwa kunaswa katika mkanda wa video na sauti kupitia mtandao wa kiuchunguzi uliokuwa umetegwa na mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari.

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), imesema inaendelea na uchunguzi wa tuhuma dhidi ya mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti.

Mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola aliliambia gazeti hili jana kuwa uchunguzi unaendelea baada ya kukamilika hatua nyingine zitafuata.

Mnyeti ambaye kabla ya kutuhumiwa kutoa rushwa alikuwa ni mkuu wa wilaya ya Arumeru, anadaiwa kunaswa katika mkanda wa video na sauti kupitia mtandao wa kiuchunguzi uliokuwa umetegwa na mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari.

Oktoba mosi, Nassari na Godbless Lema (mbunge wa Arusha Mjini) walipeleka ushahidi ambao unawatuhumu madiwani 10, kuhama katika chama hicho kwa kupewa rushwa huku wakiomba Rais John Magufuli kuchukua hatua ili kukomesha vitendo hivyo.

Nassari alisema katika ushahidi wao, ambao wameuonyesha kwa wanahabari wakidai madiwani waliojizulu wamepokea rushwa ya fedha, ajira, posho za vikao vyote vilivyobaki na kiinua mgongo cha udiwani miaka mitano na kulipiwa mkopo wa benki.

Kuhusu matumaini ya kukamilika kwa uchunguzi huo, Mlowola alisema: “Muda wa sheria kwa uchunguzi unaendelea tukikamilisha hatua nyingine zitafuata.”

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti viongozi hao walikana tuhuma hizo, katibu tawala wa wilaya ya Arumeru, Timoth Mzava ambaye alionekaa katika video hiyo, alisema ameufuatilia ushahidi unaozungumzwa na wabunge hao na kubaini kuwa ni wa kuungaunga na hauna ukweli wowote.