Takukuru yachunguza Sh10 milioni za wabunge CCM

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola.

Muktasari:

Wiki iliyopita, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), Freeman Mbowe wakati akiuliza swali kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliibua tuhuma dhidi ya wabunge hao akidai kwamba walipewa fedha hizo ili wapitishe mpango wa maendeleo ya Taifa na muswada wa Sheria za Huduma za Habari.

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) imeanza kuchunguza tuhuma za wabunge wa CCM kupewa Sh10 milioni kila mmoja ili kupitisha Muswada wa Sheria za Huduma za Habari.

Wiki iliyopita, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), Freeman Mbowe wakati akiuliza swali kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliibua tuhuma dhidi ya wabunge hao akidai kwamba walipewa fedha hizo ili wapitishe mpango wa maendeleo ya Taifa na muswada wa Sheria za Huduma za Habari.

Hata hivyo, swali hilo halikujibiwa na Waziri Mkuu baada ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kumkingia kifua akidai swali hilo halikuwa la kisera.

Mbowe licha ya kusisitiza kwamba swali hilo ni la kisera kwa sababu masuala ya rushwa na maadili ya viongozi wa umma ni ya kisera, aligonga mwamba.

Suala hilo liliibuka tena kwenye mahojiano kati ya Rais John Magufuli na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, na Rais alisema vyombo vinavyohusika vinalichunguza ili kupata ukweli.

“Ninafahamu kuna kanuni za Bunge na nina uhakika vyombo vya PCCB (Takukuru) vitauliza kupata ushahidi. Tuna vyombo vyetu vinavyoshughulikia rushwa, bahati nzuri sheria sasa imeshapitishwa, sheria namba 3 ya mwaka 2016, watakwenda kuthibitisha huko,” alisema Rais Magufuli wakati akijibu swali la Henry Mhanika ambaye ni Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (Moat).

Akizungumzia suala hilo jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola alisema wameanza kufanya uchunguzi juu ya suala hilo kwa sababu ni jukumu lao na watalifanya kiuhakika.

Alisema: “Kama Rais amesema tunachunguza suala hilo, mnataka mimi niseme nini? Ndiyo, tumeanza kuchunguza, Takukuru ni chombo chake na tumeanza kazi hiyo. Kama na wewe una ushahidi tuletee tuufanyie kazi.”

Alipoulizwa kama analifanyia kazi suala hilo, Kamishna Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda alisema: “Takukuru ndiyo wenye kazi hiyo kwa sasa, watafute uwaulize.”

Hata hivyo, muswada wa habari ulipitishwa na Bunge Jumamosi iliyopita licha ya kupingwa na wadau mbalimbali wa tasnia ya habari na wabunge wa upinzani.

Wachambuzi mbalimbali wamezungumzia tuhuma hizo kwamba zimelichafua Bunge na kuhatarisha uhuru wa chombo hicho, ambacho kina dhamana kubwa ya kutunga sheria zinazoongoza Taifa hili.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Faraja Kristomus alisema tuhuma hizo ni nzito kwa chombo cha kutunga sheria na kwamba siyo mara ya kwanza kutolewa kwa tuhuma za rushwa kwa wabunge.

Alisema tuhuma hizo zinaibua maswali mengi ikiwamo hamu ya wananchi kutaka kujua kama kweli wabunge walipokea Sh10 milioni, na kama ndiyo jumla ya fedha zilizotolewa ni kiasi gani na fedha hizo ni za nani kati ya CCM au Serikali.

“Inabidi Bunge lichunguze na kutoa majibu kuhusu suala hili, nashindwa kusema moja kwa moja kwamba muswada huo umepita kwa sababu ya rushwa hiyo, lakini safari hii wabunge wa CCM wameonekana kuungana sana ukilinganisha na mabunge yaliyotangulia,” alisema.

Alisisitiza kwamba uongozi wa Bunge usilifumbie macho suala hilo hata kama liliulizwa nje ya kanuni kwa sababu linatoa picha kwamba wabunge wote ni wala rushwa na hilo litafanya sheria hiyo isipokelewe na wananchi kama sheria halali.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema Takukuru inatakiwa kuzifanyia kazi tuhuma hizo kwa sababu ni rushwa kama yalivyo matukio mengine ya rushwa.

Alisema endapo itabainika kwamba tuhuma hizo ni za kweli, wananchi watakosa imani na Bunge lao kwa sababu litakuwa limeshindwa kutumia uhuru wake katika kufanya maamuzi yenye manufaa kwa Taifa.

“Tusubiri tu taarifa ya vyombo vinavyofanya uchunguzi, hapo ndiyo tutapata ukweli wote. Inawezekana pia zikawa ni siasa ndani ya Bunge, lakini uchunguzi ni muhimu kwa sababu lisemwalo lipo,” alisisitiza Profesa Mpangala.