Tamu na chungu ya matumizi ya EFD

Muktasari:

  • Tangu alipoingia Ikulu Novemba 5, 2015, Rais Magufuli amekuwa akikunjua makucha yake katika makundi yanayotakiwa kutumia mashine za kielektroniki za kutoza kodi (EFD).

Kila jukwaa analosimama akitoa maagizo, kuonya, kuwajibisha au kutoa maelekezo yoyote, Rais John Magufuli hakosi kuwakumbusha wafanyabiashara kutoa na Watanzania kudai risiti.

Tangu alipoingia Ikulu Novemba 5, 2015, Rais Magufuli amekuwa akikunjua makucha yake katika makundi yanayotakiwa kutumia mashine za kielektroniki za kutoza kodi (EFD).

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), makundi yanayoguswa zaidi na EFD ni wafanyabiashara wa maduka ya vipuri, mawakili, maduka ya jumla, wafanyabiashara wakubwa wa mbao, migahawa mikubwa, maduka ya simu na vipuri vyake, baa na vinywaji baridi, studio za picha, huduma za vyakula katika matukio ya sherehe, wauzaji wa pikipiki, maduka makubwa ya nguo na biashara zinginezo.

Hata hivyo, kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita joto la mashine hizo limeonekana kupitia ukaguzi wa kundi la wafanyabiashara wa vituo vya mafuta, maduka makubwa ya bidhaa, usafirishaji wa abiria mikoani, migahawa mikubwa.

Tayari TRA imeshavifungia vituo 241 vya mafuta ambavyo havitaruhusiwa kufanya biashara hadi vitakapofunga mashine za EFD.

Lakini vituo vingine 840 vimepewa muda hadi Agosti 31 kuhakikisha vimekamilisha kufunga mashine hizo, vingine vitafungwa pia. Kampeni ya ukaguzi huo ni ‘kagua utoaji risiti na kudai risiti’.

Matokeo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la siku 14 la Rais Magufuli la kuvifungia vituo vyote vya wafanyabiashara wa mafuta wanaokwepa kufunga EFD katika vituo vyao.

Akiwa katika uzinduzi wa barabara ya Kigoma-Biharamulo-Lusahunga, Rais Magufuli alisema ni bora Taifa likose mafuta kwa muda kuliko kuwavumilia wakwepa kodi.

Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanasema utamaduni wa kukwepa kodi au kutojali umuhimu wa kodi unaweza kuvunjwa na kuongeza hamasa ya ulipaji kodi kwa hiari ili Taifa lijitegemee na kuepuka mitego ya misaada iliyo na masharti kutoka kwa wahisani.

Meneja wa kituo cha mafuta cha MPS kilichopo Msasani ambaye hakutaka jina lake kutajwa anaunga mkono ulipaji kodi kwa kutumia mashine hizo na anakiri TRA imeshampiga faini ya Sh4.5 milioni kwa kutotoa risiti ya huduma hiyo Mei, mwaka huu.

Meneja huyo anasema njia wanazotumia TRA ni kujificha na kamera umbali wa mita chache kutoka kwenye kituo cha mafuta kabla ya kujitokeza.

“Hatari iliyopo ni kwamba, faini hizo zinawahusu hata wale wasiotoa risiti kwa mafuta ya Sh10,000. Pia elimu wanakupa ukiwa tayari umeshapigwa faini badala ya kukupa elimu kwanza, kwani TRA inatoa elimu kwa vyombo vya habari tu, siyo wote tunaangalia vipindi vya televisheni, hili wangerekebisha,” anasema.

INAENDELEA UK 26

INATOKA UK 25

Meneja wa Kituo cha Total kilichopo Magomeni jijini Dar es Salaam, Fatma Ali anasema kila baada ya siku sita hadi saba maofisa wa TRA wamekuwa wakipita kufanya ukaguzi.

“Kulipa kodi ni suala zuri kwa sababu inatumika kwa maendeleo ya nchi, lakini taarifa ya bei za TRA zinachelewa kubadilika katika risiti kwa mfano, bei inaposhuka risiti zinatoka na bei ya zamani,” anasema Fatma.

Kuhusu hoja ya elimu, Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipa Kodi kwa Umma wa TRA, Richard Kayombo anasema ukaguzi huo ulizinduliwa Juni, wakibandika stika katika maeneo ya biashara kote nchini ili watu wapate taarifa. Anasema anayekamatwa anatakiwa alipe haraka.

Pia, anasema jukumu la mteja ni kuangalia tarehe kwenye risiti kama ni sahihi na malipo yaliyoandikwa ni halisi katika risiti.

Kayombo anasema katika ukaguzi huo endelevu ulioanza Julai, endapo kuna mteja au muuzaji ataonekana kuwa na matatizo sugu atapandishwa mahakamani.

Mtego wa wamachinga

Mhadhiri mwandamizi wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja anasema Rais Magufuli yupo katika mtego wa wafanyabiashara wadogo wa bidhaa maarufu kama wamachinga, baada ya kuwaruhusu kufanya biashara katika maeneo yoyote.

“Hawa ni bomu la kisiasa, kiuchumi na kijamii. Ni wengi baadhi yao wanauza bidhaa zisizokuwa na ubora, hazina uhalali, hazina utambulisho kwenye soko na hawana EFD,” anasema Profesa Semboja.

“Kisiasa hao (wamachinga) wanaweza kukwamisha hata ndoto za uchumi wa viwanda kwani wataviua, kwa sababu viwanda vingine itabidi vianze kujiendesha kiujanja ujanja ili kuleta ushindani wa masoko.”

Profesa Semboja anasema athari nyingine ni hofu ya kupungua kwa idadi ya wawekezaji kutoka nje ambao hawatakuwa tayari kuja kuendesha soko la ushindani wa bidhaa zisizokuwa na uhalali kisheria.

Mtego mwingine, anasema ni idadi kubwa ya Watanzania kutokulipa kodi huku wachache wakilipa. Anasema wastani wa asilimia 40 ya kodi inayokusanywa na TRA inatokana na uingizaji wa bidhaa nchini kupitia bandari, wastani wa asilimia 40 pia hukusanywa kutoka kwa walipa kodi wakubwa ambao ni wazalishaji wa njia ya viwanda na kampuni.

“Sasa asilimia takribani 20 inayobaki inatakiwa kukusanywa katika kundi la wafanyabiashara wadogo, (wakiwamo wamachinga na wengineo) ambao ni karibu asilimia 80 ya walipa kodi wote, lakini katika taarifa za TRA inaonyesha karibu asilimia nne tu ndiyo wanaolipa kodi hadi sasa. Ni hatari sana wachache kulipa zaidi na wengi walipe kidogo au wasilipe kabisa,” anasema Profesa Semboja.

Tatu, anasema changamoto nyingine ni kukosekana kwa utayari wa walipa kodi katika matumizi ya EFD, tofauti na ilivyokuwa awali katika mfumo wa makadirio.

“Zamani mfanyabiashara alikadiriwa wakati mwingine ujanjaujanja ulitumika kidogo lakini sasa ni njia ya kisayansi, kuna wapya wanaoanza kutumia na wengine waliokuwa wanatumia ukadiriaji, siyo rahisi kubadilika upesi lakini muhimu Serikali ingegawa bure hizo mashine kwa makubaliano fulani,” anasema.

Operesheni EFD

Pamoja na hatua hizo, TRA inaendelea na ukaguzi wa matumizi ya mashine hizo nchi nzima, ikitoa faini na kufungia biashara za wakwepaji wa mashine hizo. Kwa mujibu wa TRA, mteja atakayenaswa hana risiti atatozwa faini inayoanzia Sh300, 000 hadi Sh1.5 milioni na muuzaji asipotoa stakabadhi atatozwa faini inayoanzia Sh3 milioni hadi Sh4.5 milioni.

TRA imeshafanya operesheni za EFD kwa baadhi ya wahusika. Juni mwaka huu, TRA kupitia maofisa wa Kampuni Yono iliyopewa dhamana na TRA ya kukamata mali za wadaiwa sugu na wakwepa kodi, ilifungia baadhi ya maduka eneo la Kariakoo, yaliyokuwa hayatumii mashine hizo kabla ya kulipa faini ili kuendelea tena na biashara.

Mei mwaka huu, TRA katika Mkoa wa Ilala jijini Dar es Salaam, vilevile kupitia Yono ilikamata magari zaidi ya 300 ambayo wahusika wake wanadaiwa kodi na Serikali. Katika kipindi cha mwezi mmoja magari 14,000 yalikamatwa kabla ya kulipa kodi na kuachiwa.

Mwezi uliopita mkoani Arusha, TRA ilitoa tahadhari kwa wafanyabiashara, wakiwapo wamiliki wa baa na nyumba za kulala wageni, wakitakiwa kutumia EFD ili kuepuka adhabu.

Mbali na maeneo hayo, Rais Magufuli tayari ameshakunjua makucha yake katika kampuni za simu na mabasi ya abiria mikoani nchi nzima baada ya kuingiza teknolojia mpya ya kutambua na kukusanya mapato ya Serikali.

Matokeo ya ukaguzi huo yamekuwa ni sehemu ya ongezeko la makusanyo ya kodi kwa mamlaka hiyo kukusanya kiasi Sh14.4 trilioni kwa 2016/17.

Makusanyo haya ni sawa na ukuaji wa asilimia 7.67 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2015/16 ambayo yalikuwa ni kiasi cha Sh13.3 trilioni.

Kuhusu kodi ya majengo, Kayombo anasema mamlaka hiyo imekusanya Sh31 bilioni katika mwaka wa fedha ulioishia Juni mwaka huu.

Mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara nchini, Johnson Minja anasema changamoto nyingi zilizokuwa zikilalamikiwa na wafanyabiashara kwa sasa zimepungua na uongozi ulishatoa maagizo ya kutekeleza utumiaji wa mashine hizo.

Minja anasema changamoto zilizobakia ni pamoja na baadhi ya wafanyabiashara waliotakiwa kupewa mashine hizo bure ambao bado hawajapewa katika mikoa mbalimbali huku baadhi ya mashine zikionekana kuwa na hitilafu.

Uzuri wa EFD

Pamoja na hatua hizo, TRA inasema utaratibu wa kutumia Mashine za EFD ulianzishwa kwa lengo la kumrahisishia mfanyabiashara utunzaji wa kumbukumbu za biashara za kila siku pamoja na kuondoa usumbufu wakati wa ukadiriaji wa kodi.

Mfumo huo wa kutumia EFD ulianza kutekelezwa kwa awamu. Awamu ya kwanza ilianza mwaka 2010 kwa wafanyabiashara waliosajiliwa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat).

Awamu ya pili ilianza kutekelezwa mwaka huu 2013 ikihusisha wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa kwenye VAT lakini mauzo yao ghafi kwa mwaka ni Sh14 milioni na zaidi.

TRA, katika taarifa yake inasema kwa kundi la wafanyabiashara zisizo rasmi aina ya mamalishe, babalishe na wamachinga hawahusiki katika awamu hiyo kwa sababu hawana sehemu maalumu ya kufanyia biashara.

Hata hivyo, tayari Serikali kupitia hotuba ya bajeti kuu Julai mwaka huu, imeonyesha nia ya kuanza kuwinda kodi ya wafanyabiashara hao baada ya kuwaahidi vitambulisho maalumu vitakavyosaidia kuwatambua rasmi ili waweze kupatiwa maeneo maalumu ya kufanyia biashara.