Tanroads, TTCL kushirikiana katika huduma ya intaneti

Picha inayoonyesha jinsi mkongo wa taifa ulivyosambaa nchini

Muktasari:

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara, Mhandisi Patrick Mfungale amesema mradi huo unaotarajiwa kuongeza ufanisi kwa kiwango kikubwa, una thamani ya Sh1.1 bilioni na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12 tangu kusainiwa kwake.

Dar es Salaam. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) zimetiliana saini mkataba wa kuunganisha huduma ya mtandao wa intaneti nchi nzima kwa kutumia mkongo wa mawasiliano wa TTCL.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara, Mhandisi Patrick Mfungale amesema mradi huo unaotarajiwa kuongeza ufanisi kwa kiwango kikubwa, una thamani ya Sh1.1 bilioni na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12 tangu kusainiwa kwake.

Mfungale amesema mradi huo utakaotekelezwa katika mikoa 25 na vituo vitatu vya mizani, utatumia miundombinu ya mawasiliano ya TTCL iliyounganishwa katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB).

Ameiitaja mikoa hiyo kuwa ni Singida, Tabora, Kigoma, Tanga, Mtwara, Kibaha, Iringa, Musoma na Kagera.

Mikoa mingine ni Dar es Salaam (Keko na Mabibo), Lindi, Njombe, Mwanza, Ruvuma, Manyara, Shinyanga, Dodoma, Mbeya, Sumbawanga, Simiyu, Arusha, Rukwa, Kilimanjaro, Geita na Morogoro.