Thamani mauzo ya hisa yapungua DSE

Muktasari:

Wiki mbili zilizopita, benki za biashara zilitoa taarifa za hesabu zao za fedha kwa robo ya pili ya mwaka huu na kuonyesha kuwa faida ilipungua.

Dar es Salaam. Thamani ya mauzo ya hisa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa wiki iliyoishia Agosti 11 imepungua licha ya idadi ya zilizouzwa kuongezeka.

Wiki mbili zilizopita, benki za biashara zilitoa taarifa za hesabu zao za fedha kwa robo ya pili ya mwaka huu na kuonyesha kuwa faida ilipungua.

Faida baada ya kodi ya Benki ya NMB ilipungua na kufikia Sh35.293 bilioni kwa robo ya pili ya mwaka huu ikilinganishwa na Sh45 bilioni za robo ya pili ya mwaka jana.

Pia, faida ya baada ya kodi ya Benki ya CRDB ilipungua na kufikia Sh13.3 bilioni kwa robo ya kwanza ya mwaka huu ikilinganishwa na Sh27.473 bilioni ya muda kama huo kwa mwaka jana.

Katika wiki iliyoishia Agosti 11, Kampuni ya Bia Tanzania iliongoza kwa mauzo ya asilimia 90 ikifuatiwa na CRDB iliyokuwa na asilimia saba.

Bei ya hisa za CRDB zilianza kushuka Agosti Mosi na kuhusishwa na kutangazwa kwa ripoti yao ya fedha ya mwaka iliyoonyesha kupungua kwa faida kwa kiasi kikubwa.

Agosti Mosi bei ilishuka kwa Sh5 kutoka Sh210 hadi Sh205. Bei hiyo iliendelea kushuka na Agosti 3 hisa moja iliuzwa kwa Sh200 kabla ya kufikia Sh195 kwa hisa kulingana na taarifa ya Agosti 11.

Taarifa ya fedha ya mwaka ya benki hiyo inaonyesha kupungua kwa faida kwa zaidi ya nusu.

Mwaka jana faida baada ya makato ya kodi ilikuwa ni Sh27.47 bilioni lakini mwaka huu imekuwa Sh13.3 bilioni.

Hata hivyo, taarifa ya DSE inaonyesha idadi ya hisa zilizouzwa imeongezeka kutoka hisa 600,000 wiki iliyoishia Agosti 4 hadi hisa milioni 1.4 kwa Agosti 11.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Udalali ya Orbit Securities, Simon Juventus alisema suala la kuporomoka kwa bei ya hisa za CRDB ni jambo la kawaida linalotokana na uhitaji sokoni na wala haihusiani na ripoti ya fedha mwaka inayoonyesha kushuka kwa faida.

“Suala la kupungua kwa faida kwa mwaka huu sio tatizo la benki moja tu bali sekta nzima ya benki na fedha. Sio anguko kubwa. CRDB imeanza mwezi vibaya lakini huenda ikamaliza vizuri bado watu wana imani nayo kutokana na hisa zake kuuzwa kwa bei ndogo ambayo wengi wanaweza kuimudu,” alisema Juventus.

Pia, ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa katika soko umepungua kwa Sh524 bilioni kutoka Sh18.3 trilioni kwa wiki iliyoishia Agosti 4 hadi Sh17.7 trilioni.

Ukubwa wa mtaji wa kampuni za ndani nao pia, umepungua kutoka Sh7.7 trilioni hadi Sh7.6 trilioni.

Taarifa ya DSE inaeleza kushuka kwa ukubwa wa mitaji ya kampuni zilizoorodheshwa kunatokana na kushuka kwa bei za hisa za Shirika la Ndege la Kenya kwa asilimia 22, Uchumi Supermarket Limited asilimia 14, Kampuni ya Bia ya Afrika Mashariki asilimia 8 na Benki ya CRDB kwa asilimia 5.