Timuatimua CCM imechochea tanuri

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka mkoani Mwanza wakishangilia walipokuwa wakitambulishwa baada ya kuanza kwa kikao maalum kilichofanya kazi ya kupitisha mabadiliko ya Katiba na kanuni za chama hicho mjini Dodoma juzi. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Moto huo umemuunguza kisha kumtupa nje ya chama, kigogo mwanamke wa chama hicho, Sophia Simba, ambaye alikuwa kiongozi wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) kwa mihula miwili, mbunge wa viti maalumu na mjumbe wa Kamati Kuu.

Dar es Salaam. CCM imechochea moto mkali kwa wanaoitwa wasaliti, ambao hawakukubaliana na uamuzi wa mamlaka za chama kuelekea kumpata mgombea urais wa chama hicho mwaka 2015.

Moto huo umemuunguza kisha kumtupa nje ya chama, kigogo mwanamke wa chama hicho, Sophia Simba, ambaye alikuwa kiongozi wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) kwa mihula miwili, mbunge wa viti maalumu na mjumbe wa Kamati Kuu.

Mbali na Simba ambaye aliongoza wizara mbili; Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Jinsia na Watoto na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne, mwingine aliyefukuzwa uanachama ni Mwenyekiti wa CCM wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida.

Wengine ni wenyeviti wa CCM wa mikoa, Jessica Msambatavangu (Iringa), Erasto Kwilasa (Shinyanga) na Christopher Sanya wa Mara.

Miongoni mwa waliofukuzwa uanachama wamo wenyeviti watano wa wilaya, wajumbe wawili wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), jumla yao ikiwa 12, huku wengine wakiondolewa uongozi na kubakizwa kwenye chama na baadhi kupewa onyo kali.

Hata hivyo, hali hiyo inaweza ikatafsiriwa kuwa ni ukandamizaji wa upepo wa kidemokrasia maana yake ni kuminya sauti za wengi. Watu wanaweza kunyamaza wanapominywa kwa sababu za woga, ila mtu huru hupaswa kuzungumza.

Uongozi wa juu uliopita wa CCM, kupitia kamati zake ndogo mbili, ya Maadili na ile ya Wazee, walikata jina la Edward Lowassa, kwa hiyo halikufikishwa hata kwenye mkutano wa Kamati Kuu kuchuja wagombea.

Nchimbi, Simba na Kimbisa walitoka na kueleza kutoridhishwa na uamuzi uliofanywa wa kukatwa kwa majina ya wagombea, akiwamo Lowassa. Hii ndiyo haki ya kidemokrasia.

Gharama ya demokrasia ni kuheshimu hata wanaopingana na uamuzi wa chama. Kwamba waachwe waseme kufikisha hisia zao. Hiyo ndiyo demokrasia kwenye chama. Kutaka watu wasiseme ni kuwajengea woga.

Habari zaidi Soma Mwananchi