Treni ya umeme kuanza Desemba mwakani

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akionesha nakala ya Jarida la Nchi Yetu Tanzania linalotolewa na Ofisi yake, ambalo limeainisha mafanikio mbalimbali ya kijamii na kiuchumi yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka mitatu madarakani (2015-2018). Mkutano huo umefanyika leo Jumatatu Novemba, 2018.

Muktasari:

  • Leo Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imetimiza miaka mitatu tangu ilipoingia madarakani huku Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas akielezea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho

Dar es Salaam. Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas amesema mwaka ujao treni ya kwanza ya umeme itaanza safari baada ya kukamilika kwa ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge).

Amesema utekelezaji wa mradi wa reli hiyo inayoanzia bandari ya Dar es Salaam hadi mji mkuu Dodoma na baadaye hadi nchi za jirani za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umekamilika kwa asilimia 30.

Akizungumza leo wakati akielezea miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano tangu Rais John Magufuli alipoingia madarakani, Dk Abbas alisema ujenzi wa reli hiyo ni kati ya mafanikio makubwa ambayo wengi hawakuamini kama yanawezekana kwa kutumia mapato ya ndani.

“Katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Magufuli Serikali imesimama kwenye baadhi ya mambo makubwa ambayo wengi walidhani haiwezekani, tumeahidi na tumetekeleza,” alisema.

Ametaja miradi mingine mikubwa iliyotekelezwa katika kipindi hicho kuwa ni ununuzi wa ndege saba, nne zikiwa tayari zimewasili, ujenzi wa barabara ya juu ‘fly over’ ya Mfugale katika eneo la Tazara na ujenzi wa mradi wa umeme wa Stigler’s George ambao upo kwenye mchakato.

Dk Abbas alisema katika kipindi hich, Tanzania imeendelea kuenzi amani na kwamba kama ingekosekana ujenzi wa miradi yote usingefanikiwa.

Pamoja na hayo, Dk Abbas alisema Rais Magufuli amefanikiwa kusimamia falsafa ya kuenzi misingi ya kuanzishwa kwa taifa ikiwamo kujitegemea, maendeleo, uhuru na amani.