Tuhuma za wizi wa kuku 80 zilivyovunja ndoa Chamwino

Muktasari:

  • Yote hayo yapo kwa Veronika Petro Madeje (34) mkazi wa Kijiji cha Mloda Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ambaye anatamani kama asingezaliwa kuliko ilivyo sasa maisha yake kuwa magumu huku jasho lake likitumiwa na wengine.

Ni simulizi iliyojaa huzuni na sononeko lakini wanaoonewa huruma zaidi ni watoto wasio na uwezo wa kupambana na hali ngumu ya maisha inayotokana na kutengana kwa wazazi wao.

Kuna usemi usemao “lala maskini amka tajiri” kinyume chake “lala tajiri amka maskini.”

Yote hayo yapo kwa Veronika Petro Madeje (34) mkazi wa Kijiji cha Mloda Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ambaye anatamani kama asingezaliwa kuliko ilivyo sasa maisha yake kuwa magumu huku jasho lake likitumiwa na wengine.

Simulizi ya mama huyu mwenye watoto saba ni kama mchezo wa kuigiza lakini ni tukio la kweli lililotokea.

“Niliambiwa nimeiba kuku 80, niliacha ng’ombe 200 na mbuzi wengi sijui idadi yake, lakini mwenzangu ametumia mali hizo kuoa wake wawili mimi nalala njaa,” ndipo inapoanzia.

Historia ya Veronica

Veronika alizaliwa katika Kijiji cha Mloda (1974) akasoma kijiji hapo hadi darasa la saba, hakubahatika kuendelea na masomo ya juu ndipo akaolewa na Jeu Ndalu Miyoyi.

Wawili hawa walioana na kuanza maisha katika Kijiji cha Iwondo Wilaya ya Mpwapwa ambako Mungu aliwajalia kupata watoto wanane (mmoja alifariki dunia), lakini kwa sasa mkubwa ana umri wa miaka 19 (ameolewa) na wadogo wawili (pacha) wakiwa na umri wa miaka miwili.

Katika kujishughulisha na kilimo walibahatika pia kuwa na mifugo wakiwemo ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku ndani ya nyumba kisha wakajenga nyumba nzuri kijijini hapo.

Ilikuwa mwaka 2015 ndipo maisha ya wawili hawa yalipoanza kuingia uchungu na hali ikawa mbaya kabla ya mmoja kujikuta akipiga miayo kwa njaa na wala asijue kesho yake itakuwaje.

INAENDELEA UK 16

INATOKA UK 15

Ugonjwa wa mdondo chanzo

Vero anasema wakati mmoja uliibuka ugonjwa wa kuku unaojulikana kama mdondo ambao uliwashambulia kuku wengi kijijini kwao hata kufikia hatua ya kuwamaliza kabisa.

Wakati hayo yakitokea, maisha yao hayakuwa na hitilafu ya aina yoyote na mumewe alikuwa anaishi pembezoni mwa kijiji ambako walikuwa wameweka boma la mifugo yao.

“Nilituma watoto wakampelekea taarifa kuwa kuku wanakwisha na yeye akaagiza nyama kwa wale waliokuwa wanakufa tukawa tunampelekea lakini akasema hawezi kununua dawa ya kuwatibu kwani isingewezekana,” anasimulia Veronica.

Anabainisha kuwa nyumbani kwao walikuwa na kuku wasiozidi 20 na walikufa 18 wakabaki wawili wadogo na kwamba kutokana na imani yao iliwaruhusu kuwala nyama kuku waliokufa na walifanya hivyo kwa kushirikisha.

Hali iligeuka ghafla

Haikumbuki siku lakini majira ya jioni mumewe alirudi na kumuuliza kuku walikopelekwa lakini alipojibiwa kuwa wamekufa na ugonjwa na nyama alikuwa akimpelekea akabadirika ghafla.

“Akasema haiwezekani, haiwezekani na haitawezekana kuku wafe wote halafu nisiwe na taarifa ndipo akaanza mikwara na vipigo vikaanza siku hiyo,” anasema huku akifuta machozi.

Kwa mujibu wa Veronica, hakuamini kama jambo hilo lingeweza kufika mbali lakini siku iliyofuata alifukuzwa nyumbani kwake na akiambiwa ni mwizi wa kuku na kuwa alikuwa ameiba kuku 80 hivyo hatakiwi kwa mumewe tena ama kuwarudisha na akishindwa ndiyo tiketi ya kuondoka nyumba hiyo.

Aliondoka asubuhi na mapema kurudi kwao, lakini walipojaribu kurudi akiwa na ndugu zake walikuta tayari mumewe amekwishafika Mahakama ya Mwanzo Chipogolo na kumshtaki kwa wizi wa kuku 80.

Anasimulia kuwa ilikuwa ni mshituko kwake kwani hakujua namna kesi ilivyokuwa inaendeleshwa na hakujua tarehe za kesi lakini yote yakachangia kesi kubanwa zaidi upande mmoja kabla ya kutiwa hatiani.

“Ukweli hatukuwahi kuwa na kuku hata 30, hao nilioiba sijui walikuwa wametoka wapi na niliwauza wapi wote…..yaani (anafuta machozi)… unajua hadi leo siaminiki kwamba naitwa mwizi wa kuku wakati ndiyo kwanza nilikuwa natoka kujifungua hawa pacha wangu na mahitaji yote mume wangu alikuwa ananipa sasa ningeiba wa nini?” anahoji.

Kilichofuata

Veronica anasema baada ya hapo ndugu zake walimshauri kuwa mumewe amekuwa si mwema kwani kama aliweza kumwambia ameiba kitu ambacho hawakuwa nacho huenda ungefika wakati akawa na jambo kubwa zaidi.

Hapo ndipo harakati za kupeana talaka zilipoanza na safari zilianza tena mahakamani kwa ajili ya wawili hao kuachana na kila mmoja kujua hamsini zake.

Mama huyu ambaye wakati wote anaonekana kuwa na huzuni anasema ulifika wakati ambao alilazimika kudai talaka na Mahamakana ilikubali kuwaachanisha.

Apewa mali

Kinachomuuma ni mgao uliotolewa na Mahakama ambapo mumewe alikiri kuwepo ng’ombe 200 lakini Mahakama ya mwanzo iliamuru mama huyu apewe ng’ombe sita na mbuzi watano kisha abaki na watoto watatu.

Anasema hakuamini kilichotokea katika uamuzi wa Mahakama na alipewa mifugo hao lakini alipouliza kulikoni hakupata majibu ikiwemo nyumba kubwa waliojenga pamoja zaidi ya kuambiwa kama hakuridhika akate rufaa.

Hata hivyo, mahakama ilimwamulu Jeu kuendelea kutoa matunzo kwa watoto watatu ambao wako chini ya umri wa miaka saba jambo ambalo Veronica anakiri amekuwa akitekeleza kama alivyoelekezwa kwa kutoa nafaka lita 20 na Sh30,000 kila mwezi.

Kwa sasa Veronica hana nyumba, hana shamba la kulima, hana biashara ya aina yoyote kama ilivyokuwa alipokuwa kwa mumewe kwani alikuwa akijishughulisha na biashara ndogo ndogo na hivyo kuyafanya maisha yake kuwa magumu zaidi hivi sasa.

Hata hivyo, tatizo limeongezeka baada ya mumewe kuwafukuza watoto watatu aliokuwa anaishi nao kwa amri ya Mahakama kwa kile kinachodaiwa ni wake zake kuwakataa.

Simulizi ya mtoto

Hamisi Ndalu (17) ambaye ni mtoto wa pili kwa familia ya wanandoa hao anasema maisha yao yalikuwa magumu baada ya mama yake kuondoka nyumbani.

“Tulikuwa na mifugo ambayo mama aliiacha lakini baba akachukua ng’ombe 30 akaoa mke baada ya muda mfupi alichukua tena ng’ombe wengine 28 akaoa mke wa pili yaani sisi tukawa na kazi ya kujipikia lakini kila siku ni kuchunga na hakuna mtu wa kwenda shule,” anasema Hamisi.

Kijana huyu anasema ulifika wakati baba yao akawa mkali kila anaporudi kutoka matembezi na hakutaka kusikia chochote alichoombwa na watoto wake ambao muda wote aliwaacha kuendelea kuishi nyumba ya mama yao.

Anasema hali ya maisha iliendelea kuwa mbaya zaidi lakini ulifika wakati baba yao akasema Hamisi na wenzake wamekuwa na kiburi ndipo akawafukuza na kuwachomea nguo zote wakaenda kushitaki kwa mwenyekiti wa kitongoji lakini baba yao akawageuzia kibao kuwa walitaka kumpiga.

Mume asimulia

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka kijijini kwao Iwondo, Jeu alikiri Veronica ni mke wake na kwamba alimfukuza kutokana na kile alichosema anatabia mbaya na haambiliki.

“Kweli mimi niliamua kumtimua na Mahakama ilishatugawia kila kitu, kwa sasa mimi nina wake zangu wawili ambao niliwaoa baada ya yeye kuondoka lakini wenzake naishi nao vizuri,” anasema Jeu.

Anakiri pia kuwafukuza watoto nyumbani kwani walianza tabia mbaya na hata walitaka kumpiga. “Siwataki tena hapa kwangu na sihitaji kuishi nao maana wanaweza kunipiga, wale watoto wanatabia mbaya kama za upande wa mama yao.”

Kuhusu mifugo anasema iliyobaki ni yake na waliokwenda huko nao wakatafute ya kwako na mama yao lakini kwa wale wa chini ya umri anasema ataendelea kupeleka matunzo kama Mahakama ilivyoagiza huku akikiri kuwa maisha ya watoto wake ni magumu na kulala na njaa huko ni jambo la kawaida.

Mwanasheria atilia shaka

Mwanasheria kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Denis Bashaya anasema bado kuna kesi ya kuangalia hasa katika suala la matunzo ya watoto.

Bashaya hapingani na suala la mgao wa mali akisema huenda viko vigezo vilivyoangaliwa na kuamliwa mgao wa aina hiyo, lakini akasema suala la watoto bado wanayo haki ya kuomba waishi kwa nani kutokana na namna wanavyoona usalama wao.

Anamshauri Veronica kuonana na wataalamu wa ustawi wa jamii ili waweze kumpa ushauri zaidi wa namna gani afanye ili aweze kuishi kwa amani na watoto wake.

Ofisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi, Amina Mafita anasema watoto waulizwe kama wanataka kuishi kwa baba au kwa mama na vyovyote itakavyokuwa baba ataendelea kuwajibika.