Tume ya Lukuvi yakamilisha kazi yake mgogoro wa ardhi Magwegele

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi

Muktasari:

Kwa miaka zaidi ya 20 yamekuwa yakitokea mauaji ya wakulima na wafugaji katika vijiji hivyo huku mamlaka mbalimbali zikishindwa kutatua mgogoro wilayani Kilosa.

Dar es Salaam. Tume ya kijaji iliyoundwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuchunguza mgogoro wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji wa kijiji cha Mabwegele na vijiji jirani  imemaliza kazi na kutoa mapendekezo kwa waziri namna ya kuumaliza mgogoro huo.

Kwa miaka zaidi ya 20 yamekuwa yakitokea mauaji ya wakulima na wafugaji katika vijiji hivyo huku mamlaka mbalimbali zikishindwa kutatua mgogoro wilayani Kilosa.

Miezi miwili iliyopita Lukuvi aliunda tume hiyo iliyoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu kitengo cha Biashara,Jacob Mwambegele ambaye amekabidhi ripoti kwa waziri.

Akizungumza leo Lukuvi amesema mapendekezo yaliyotolewa na tume hiyo ya kijaji ndiyo yatakuwa ya mwisho.

Alisema Serikali itakuwa ikifanya uamuzi kwa kufuata maelekezo ya tume hiyo kama sheria inavyosema.

Hata hivyo Lukuvi alikataa kuzungumzia mapendekezo yaliyo kwenye ripoti hiyo akisema ataitoa mara baada ya kuisoma na kuielewa vizuri.