Tume ya Madini yashtushwa makusanyo Mirerani kushuka

Muktasari:

Utoroshaji wa madini umesababisha kushuka fedha za mrabaha kutoka Sh444 milioni hadi Sh40 milioni kwa mwezi.

Arusha. Tume ya Madini iliyoundwa na Rais John Magufuli imebaini utoroshwaji wa Tanzanite katika migodi ya Mirerani licha ya ujenzi wa ukuta kuizunguka.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Profesa Idris Kikula alisema jana kuwa utoroshaji wa madini umesababisha kushuka fedha za mrabaha kutoka Sh444 milioni hadi Sh40 milioni kwa mwezi.

Profesa Kikula aliyasema hayo jana kwa wanahabari wakati akitoa taarifa baada ya ziara ya tume katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro,

Alisema katika ziara hiyo ya Mirerani wamebaini kuwapo udanganyifu wa madalali wanaokwenda kununua madini migodini. “Madalali hawa wakitoka kununua madini wamekuwa wakipita getini, baadhi wanahofiwa kuficha madini hasa kutokana na kukosekana vifaa vya kisasa vya upekuzi,” alisema Profesa Kikula.

Alisema katika geti kuu la kuingilia na kutokea migodini hakuna vifaa vya upekuzi, badala yake hupekuliwa kwa mikono.

“Tumeshauri kujengwa eneo maalumu la madalali wote kukaa na kununua madini ili Serikali ipate mrabaha badala ya kwenda moja kwa moja migodini,” alisema.

Profesa Kikula ambaye uteuzi wake ulifanywa na Rais John Magufuli Aprili 17, alisema pia wamebaini idadi kubwa ya magari na watu wanaoingia na kutoka migodini, hivyo kuwapo uwezekano wa udanganyifu na utoroshaji wa madini.

Akizungumzia ukuta, alisema wamebaini kuna matofali yamebakia nje ya ukuta ambayo yanaweza kutumiwa na watu wasio waaminifu kupandia kufanya hujuma migodini. Pia, wamebaini hakuna kamera ndani ya migodi inayowezesha kuwaona wanaotaka kuruka ukuta huo.

“Pembezoni mwa ukuta hakuna barabara, hivyo ni rahisi wahalifu kufanikiwa licha ya kazi nzuri inayofanywa na askari wa Suma JKT kulinda ukuta huo,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema wameshauri kujengwa barabara jirani na ukuta na kuwekwa kamera maalumu.

Wachimbaji wanasemaje?

Akizungumzia baada ya Profesa Kikula kueleza changamoto walizobaini, mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini mkoani Manyara (Marema), Sadick Mnenei alisema hana uhakika kama kuna utoroshaji wa madini, lakini anafahamu kuwa uzalishaji umepungua.

“Lazima mapato ya Serikali yashuke kwani gharama za uzalishaji zimekuwa kubwa, hivyo kupunguza uchimbaji,” alisema.

Pia Mnenei alisema hali hiyo inachangiwa na mzunguko wa fedha kupungua na mitaji kushuka, hivyo kuathiri uzalishaji.

Alisema wachimbaji wadogo walikuwa wakiazima fedha kutoka kwa wafadhili ili kuwekeza katika uchimbaji, lakini kutokana na mzunguko wa fedha kuwa mgumu uwekezaji umekuwa mdogo.

Mnenei alisema baadhi ya wachimbaji walikuwa wakipata fedha kutoka kwa wakulima, lakini nako imekuwa vigumu kutokana na kushuka kwa bei ya mazao na hasa mbaazi.

Kuhusu ukuta, alisema umekuwa na faida kwa kuwa umedhibiti utoroshwaji madini huku akiunga mkono umuhimu wa kuwa na eneo maalumu la madalali kuuza na kununua madini. “Ni vizuri kujengwa eneo maalumu, lakini kipindi hiki ni vyema waruhusiwe kuuza na kununua madini kijijini Mirerani.”

Mchimbaji madini, Joseph Kaaya aliipongeza Serikali kujenga ukuta na kudhibiti utoroshwaji madini huku akiitaka kufunga vifaa vya kisasa ili kuwabaini wahalifu katika migodi hiyo.

Ukuta wa Mirerani umejengwa kwa zaidi ya Sh4 bilioni ikiwa ni hatua ya kudhibiti utoroshwaji madini.