U-CCM wa DED Ubungo waitisha Ukawa Uchaguzi Mkuu 2020

Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni katika Ofisi ya Rais - Utumishi na Utawala Bora, Ruth Mollel

Muktasari:

  • Picha hiyo inayosambaa katika mitandao ya kijamii inamuonyesha Kayombo akiwa katika mkutano wa uchaguzi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) uliofanyika hivi karibuni huko Dodoma akiwa amevalia sare za chama hicho tawala huku kishangilia.

 Kusambaa kwa picha inayomuonyesha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED) ya Ubungo, John Kayombo akiwa amevalia sare za CCM kumeibua mjadala wa kimaadili huku Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ukieleza kutishika iwapo kutakuwa na matokeo chanya katika uchaguzi.

Picha hiyo inayosambaa katika mitandao ya kijamii inamuonyesha Kayombo akiwa katika mkutano wa uchaguzi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) uliofanyika hivi karibuni huko Dodoma akiwa amevalia sare za chama hicho tawala huku kishangilia.

Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni katika Ofisi ya Rais - Utumishi na Utawala Bora, Ruth Mollel amesema mtumishi wa umma anatakiwa kuwa ‘neutral and impartial’ (asiyependelea upande wowote na mwenye maadili) na awe tayari mara zote kutekeleza sera za Serikali ya chama chochote.

Ruth aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Utumishi, alisema lengo la dhana hiyo ni kuifanya sekta ya utumishi wa umma kuwa endelevu na kuepuka mabadiliko ya watendaji wakuu kila Serikali ya chama tofauti inapoingia madarakani.

“Serikali ya Awamu ya Tano imekiuka dhana hiyo kwa kuingiza siasa katika utumishi wa umma. Tumeshuhudia nafasi za utendaji serikalini zikitolewa kwa makada na wakereketwa wa CCM ambao baadhi hawana hata ufahamu wa uendeshaji serikalini,” alisema.

“Tumeshuhudia naibu katibu mkuu wa Tume ya Mipango akigombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, huku akiwa bado mtumishi wa ngazi ya juu serikalini.”

Alisema jambo alilofanya mkurugenzi wa Ubungo linaashiria uteuzi mbovu uliofanywa na mamlaka na kwamba, una lengo la kuvuruga chaguzi zitakazofanywa.

Ruth alisema tayari dalili zimeshaanza kujionyesha katika chaguzi ndogo zilizomalizika hivi karibuni.

Katika hotuba aliyoiwasilisha katika Bunge la Bajeti la mwaka 2017/18, Ruth alisema kati ya wakurugenzi watendaji 195 walioteuliwa hivi karibuni, 65 walikuwa wagombea wa ubunge kwenye kura ya maoni ya CCM, huku baadhi ya makatibu tawala wa mikoa na wilaya na makatibu wakuu ni wakereketwa wa chama hicho.

“Matokeo ya uamuzi huu ni kuingiza siasa katika utumishi wa umma na kupoteza weledi na ni kupanda mbegu mbaya ya ubaguzi wa kisiasa katika utumishi wa umma,” alisema.

Alihoji, “Inakuwaje kwa mfano, chama kingine kikichukua madaraka ya dola? Hali ya watumishi wenye itikadi tofauti itakuwaje? Je, naibu katibu mkuu wa Tume Mipango ambaye kura zake hazikutosha katika kugombea ubunge wa Afrika Mashariki amerudi kazini?”

Alisema kambi ya upinzani imesikitishwa na kitendo cha mkurugenzi Kayombo kuuonyesha wazi umma anachokiamini jambo ambalo ni kinyume cha utawala bora.

Alitoa mfano alipokuwa mtumishi wa umma hakuonyesha mapenzi yake kwa kuwa aliamini anawatumikia Watanzania na si wana CCM.

“Serikali iache mara moja kuteua au kuajiri watumishi kutokana na itikadi za kisiasa na badala yake ijenge utumishi wa umma wenye weledi ambao uhai wake hautegemei chama kilichopo madarakani, bali utumishi wa umma endelevu unaotumikia wananchi,” alisema.

Alipotafutwa kutoa ufafanuzi kuhusu picha yake kuonekana mitandaoni, mkurugenzi Kayombo alijibu kwa kifupi kuwa hajui lolote na ndiyo kwanza alisikia habari hizo kutoka kwa mwandishi wetu.

“Sijui lolote yaani ndiyo nasikia jambo hili kutoka kwako,” alisema Kayombo.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhani Kailima akizungumzia nafasi za wakurugenzi wa halmashauri ambao ni wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo, alisema kwa mujibu wa kanuni ya 16 ya kanuni za uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani za mwaka 2015 pamoja na kanuni ya 12 ya kanuni ya Serikali za Mitaa (uchaguzi wa madiwani) za mwaka 2015, kila mratibu wa uchaguzi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kabla hajaanza kutekeleza majukumu yake wakati wa uchaguzi atapaswa kufanya mambo matatu.

“Kwanza anapaswa kula kiapo cha kutunza siri katika fomu namba sita; kula kiapo cha kujitoa uanachama wa chama cha siasa iwapo ni mwanachama katika fomu namba saba; au kula kiapo cha kusema si mwanachama wa chama chochote cha siasa katika kipindi cha utekelezaji wa kazi za uchaguzi katika fomu namba saba,” alisema.

Pamoja na maelezo hayo ya Kailima, mwanasiasa mkongwe, Njelu Kasaka alisema hakuna mipaka kati ya utumishi wa umma na watendaji wakuu kama wakurugenzi na makatibu wakuu wa wizara.

Kasaka aliyekuwa miongoni mwa wabunge 55 walioasisi kundi la G55 lililotaka kuundwa Serikali ya Tanganyika mwaka 1993, alisema hashangazwi na vitendo vinavyoendelea ambavyo kwa mtazamo wake si sawa.

“CCM ilimpokea Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo na hakuna mamlaka yoyote inayokemea vitendo hivyo,” alisema.

Kasaka alisema, “Ninachojua mtumishi wa umma wa ngazi za juu haruhusiwi kujionyesha waziwazi kama yeye ni kada wa chama kindakindaki labda kama sasa mambo yamebadilika kwa sababu sipo huko muda mrefu, kama wamebadili naweza kusema ni sawa ila kama yapo vilevile kama nilivyoyaacha hiyo si sawa.”